MOSHI-KILIMANJARO.
Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Adam Best Simba, amesema hakuna maandamano yoyote yanayofanyika kupitia mitandao ya kijamii kama inavyodaiwa, na badala yake amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kupiga kura kuwachagua wagombea wa CCM.
Mhandisi Simba aliyasema hayo katika mkutano wa kampeni wa mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, uliofanyika Kata ya Bondeni.
Alisema wapo baadhi ya watu wachache wanaotumia mitandao ya kijamii kueneza taarifa za uongo kuhusu maandamano siku ya uchaguzi, jambo alilolieleza kuwa halina ukweli wowote.
“Niwahakikishie wananchi wote wa Moshi na Tanzania kwa ujumla kwamba hakuna maandamano yoyote, na serikali imeimarisha ulinzi wa kutosha, hivyo, jitokezeni kwa wingi bila woga kwenda kupiga kura Oktoba 29, usalama ni wa uhakika,” alisema Mhandisi Simba.
Aidha, Mhandisi Simba ambaye pia ni Meneja wa Kampeni wa CCM Moshi Mjini, alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea udiwani wa Kata ya Bondeni, Alhaji Hajji Fundi, sambamba na kuwaomba wananchi kumpigia kura Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan.
Kampeni za Uchaguzi mkuu zilianza rasmi Agosti 28, 2025, na zinatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 28, huku Oktoba 29,mwaka huu, serikali imetangaza kuwa ni siku ya mapumziko ili kutoa fursa kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika zoezi la upigaji kura kuwachagua viongozi wanaowataka.









