MWENYEKITI WA UWT MOSHI MJINI AWASISITIZA WANANCHI KUICHAGUA CCM

MOSHI-KILIMANJARO.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Moshi Mjini, Theresia Komba, amesema kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) ndicho chama pekee nchini ambacho sera zake zimejikita katika kuwaletea maendeleo Watanzania wote bila ubaguzi.

Akizungumza Oktoba 25, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la Posta, Kata ya Mawenzi, Komba alisema kuwa mambo yaliyomo ndani ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030 ni ushahidi tosha kwamba chama hicho kimejipanga kuendelea kuwahudumia wananchi kwa uadilifu na uwajibikaji.

“Wanawake na wananchi wote wenye sifa ya kupiga kura wanapaswa, ifikapo siku ya uchaguzi, kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kuwachagua wagombea wanaotokana na CCM,” alisema Komba.

Katika mkutano huo, Komba alimnadi mgombea udiwani wa Kata ya Mawenzi, Apaikunda Naburi, ambaye ni mwanamke pekee kati ya wagombea 21 wa udiwani katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, na kuwataka wananchi wa kata hiyo kumpa kura za ndiyo.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwaombea kura mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, pamoja na mgombea urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mwenyekiti huyo aliwahimiza wananchi wote kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kushiriki katika zoezi la kupiga kura, akisema kufanya hivyo ni kuchagua maendeleo na ustawi wa Taifa kupitia viongozi wa Chama cha Mapinduzi.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.