MALYA AWAHAMASISHA VIJANA MOSHI MJINI KUJITOKEZA KUPIGA KURA

MOSHI-KILIMANJARO. 

Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi Mjini, Ashraf Malya, ametoa wito kwa vijana wa Jimbo la Moshi Mjini kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, 2025, akisema hatua hiyo ni msingi muhimu wa kuchochea maendeleo na ustawi wa wananchi wa Moshi.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni za mgombea udiwani wa Kata ya Mawenzi, Apaikunda Naburi, Malya alisema ni jukumu la kila kijana kutumia haki yake ya kikatiba kwa kupiga kura na kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayoamua mustakabali wa taifa.

“Kura yako ni sauti yako. Vijana tuna wajibu wa kujitokeza na pia kuhamasishana kuhusu umuhimu wa kuwachagua viongozi wa CCM wenye maono ya kweli ya maendeleo ya nchi yetu,” alisema Malya.

Akiweka msisitizo, Malya alisema vijana wanapaswa kuendelea kuwa chachu ya mabadiliko chanya kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Aidha, Mjumbe huyo wa Kamati ya Siasa alimwombea kura Apaikunda Naburi, akiwataka wananchi wa Kata ya Mawenzi kumpa tena kura kutokana na kazi kubwa alizozifanya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

"Mgombea udiwani Apaikunda Naburi ni mtu wa maendeleo na miongoni mwa madiwani ambao hawatuletei changamoto kwenye Kamati ya Siasa ya Wilaya, mpeni kura ili aendelee kusimamia maendeleo ndani ya Kata ya Mawenzi,” alisema.

Vilevile, Malya aliwaombea kura mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, pamoja na mgombea urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi kuwachagua wagombea wa CCM ili kuendeleza jitihada za maendeleo nchini.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.