SHAYO AWAOMBA WANANCHI WAMCHAGUE ILI AKASHUGHULIKIE SHULE CHAKAVU

MOSHI-KILIMANJARO.

Mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Ibrahim Shayo, amewaomba wananchi wa jimbo hilo kumpa ridhaa ya kuwa mwakilishi wao bungeni ili aweze kushughulikia changamoto za shule chakavu na miundombinu mibovu iliyojengwa miaka mingi iliyopita.

Shayo aliyasema hayo Oktoba 25, 2025, katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika kwenye viwanja vya Ofisi ya CCM, Kata ya Majengo, ambapo alisisitiza kuwa sekta ya elimu inahitaji msukumo mpya wa maendeleo.

Alitaja shule za msingi Majengo na Shauri Moyo kuwa miongoni mwa taasisi za elimu zilizochakaa, zikihitaji ukarabati mkubwa ili kutoa mazingira bora ya kujifunzia kwa wanafunzi.

"Shule hizi zimechakaa kabisa, nipe fursa ya kuwa mbunge wenu ili niweze kuibana Wizara ya Elimu kuhakikisha fedha za ukarabati zinapatikana,” alisema Shayo huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo.

Mbali na sekta ya elimu, Shayo pia aliahidi kushughulikia changamoto za barabara, majitaka, na upatikanaji wa mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, akisema atahakikisha wanaostahili wanapata mikopo hiyo kwa wakati ili kujikwamua kiuchumi.

Katika hotuba yake, mgombea huyo aliwaomba wananchi wa Moshi Mjini kuwapigia kura madiwani wote wa CCM pamoja na kumpa kura ya ushindi Rais Samia Suluhu Hassan, akibainisha kuwa serikali yake imeleta maendeleo makubwa katika Mkoa wa Kilimanjaro.

“Rais Samia ameleta zaidi ya shilingi trilioni 1.48 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo katika Mkoa wa Kilimanjaro, ambapo Jimbo la Moshi Mjini pekee limepokea zaidi ya shilingi bilioni 233,” alisema Shayo.

Alisisitiza kuwa fedha hizo zimewezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya elimu, afya, barabara na maji, hivyo akawataka wananchi waendelee kumuunga mkono Rais Samia na Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi ujao.













Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.