DK ZEKEYA AHAMASISHA WANAWAKE KUJITOKEZA KUPIGA KURA OKTOBA 29

MOSHI-KILIMANJARO.

Aliyewahi kuwa mtia nia wa Ubunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Niever Zekeya, amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Jumatano Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni wajibu wa kikatiba na fursa muhimu ya kuchagua viongozi watakaosimamia masilahi yao.

Dk. Zekeya alitoa wito huo Oktoba 25, 2025, wakati wa mkutano wa kampeni wa mgombea udiwani wa Kata ya Mawenzi, Apaikunda Naburi, uliofanyika eneo la Posta, mjini Moshi na kumuombea kura mgombea urais wa CCM Dk Samia Suluhu Hassan, mbunge Ibrahim Shayo pamoja na wagombea wa CCM katika nafasi ya udiwani. 

Katika hotuba yake, Dk. Zekeya alimpongeza Naburi kwa kuwa mwanamke pekee kati ya wagombea 21 wa udiwani waliopitishwa na chama kugombea nafasi hiyo, akisema hatua hiyo ni mfano wa ujasiri na uthubutu wa wanawake kushiriki katika uongozi wa kisiasa.

"Uwepo wa viongozi wanawake ni muhimu kwa sababu huchochea utungaji wa sera zinazogusa maisha ya wanawake na familia kwa ujumla. Ni muhimu wanawake wakatambua nguvu waliyonayo katika kuamua mustakabali wa nchi kupitia kura zao,” alisema Dk. Zekeya.

Aidha, aliwahimiza wanawake wote katika Mkoa wa Kilimanjaro na nchini kwa ujumla kutambua mchango wao katika maendeleo ya taifa kupitia ushiriki wa moja kwa moja katika michakato ya kisiasa na uchaguzi.

Dk. Zekeya aliongeza kuwa ushiriki wa wanawake katika uchaguzi wa mwaka huu unaendelea kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za Bara la Afrika zilizopiga hatua kubwa katika kuimarisha usawa wa kijinsia na kuongeza uwakilishi wa wanawake katika nafasi za maamuzi.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.