MOSHI-KILIMANJARO.
Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Ibrahim Urio, amewataka wananchi kuchagua wagombea wa CCM kuanzia ngazi ya urais, ubunge hadi udiwani, akisisitiza kuwa chama hicho kimeonesha uwezo wa kweli wa kuwaletea maendeleo Watanzania.
Urio aliyasema hayo Oktoba 25, 2025 katika mkutano wa kampeni wa mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, uliofanyika katika viwanja vya CCM vilivyopo Kata ya Majengo, Moshi.
Akizungumza mbele ya mamia ya wakazi wa eneo hilo, Urio aliwaasa wananchi kufanya maamuzi sahihi wakati wa uchaguzi kwa kuchagua viongozi wanaojali maisha yao.
“Mnapswa kufahamu kuwa siasa ni maisha. Unapokwenda kumchagua kiongozi wa kukuongoza, lazima uchague mtu anayejali maisha yako, usimchague mtu ambaye hatakusaidia,” alisema Urio.
Katika mkutano huo, Urio pia alinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030, akieleza dira na vipaumbele vya chama hicho katika miaka mitano ijayo, endapo wananchi watakipa ridhaa ya kuendelea kuongoza nchi.
Alibainisha kuwa chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, ikiwemo Mradi wa Maji wa Same,-Mwanga-Korogwe, ambao unalenga kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa mikoa ya Kilimanjaro na Tanga.
Urio alisisitiza kuwa mafanikio hayo ni uthibitisho wa dhamira ya CCM katika kuwaletea wananchi maendeleo endelevu na huduma bora.













