VIJANA WAMUOMBEA KURA MGOMBEA UDIWANI KATA YA KALOLENI KWA MASHAIRI

KALOLENI-MOSHI.

Kikundi cha vijana katika Kata ya Kaloleni, Manispaa ya Moshi, kimetumia njia ya kipekee ya kuimba mashairi ya kisiasa kumuombea kura mgombea udiwani wa kata hiyo Nasibu Mariki kupitia Chama cha Mapinduzi CCM.

Vijana hao walitoa burudani hiyo katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika eneo la Mtaa wa Kambini Kata ya Kaloleni, ambapo walitumia mashairi yenye ujumbe wa kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na kumchagua mgombea huyo ili kuleta maendeleo katika kata hiyo.

Wakiwa wamevalia mavazi ya kijani na njano, vijana hao waliimba mashairi yaliyolenga kuonesha imani yao kwa mgombea huyo, wakisisitiza kwamba ana uwezo wa kusikiliza changamoto za wananchi, kutatua changamoto za vijana na kuleta maendeleo ya kweli katika kata hiyo.

“Tumeamua kutumia mashairi kwa sababu ni lugha rahisi inayogusa mioyo ya watu, tunataka kila mmoja aelewe kuwa tunahitaji kiongozi anayeishi na wananchi wake,” alisema Hussina Abdallah mmoja wa vijana hao.

Akizungumza baada ya burudani hiyo, mgombea udiwani wa Kata ya Kaloleni Nasibu Mariki, aliwashukuru vijana kwa moyo wao wa kujitolea, akisema hatua yao inaonesha hamasa kubwa ya mabadiliko na umoja katika kata hiyo.

“Vijana ni nguvu ya taifa, ninawashukuru sana kwa ubunifu huu nawaahidi nitakuwa diwani wa wote, nitafanya kazi kuhakikisha huduma za jamii zinaboreshwa na fursa za kiuchumi zinaongezeka kwa vijana,” alisema mgombea huyo.

Alisema akipata nafasi ya kuongoza, ataanza na utekelezaji wa miradi ya kuboresha miundombinu ya barabara za ndani, huduma za afya, usafi wa mazingira na kuanzisha vituo vya vijana kwa ajili ya ujasiriamali na michezo.

Mkutano huo ulihudhuriwa na makada wa chama hicho, wazee wa mtaa, wanawake na vijana wengi, huku hamasa ikitawala kwa nyimbo na mashairi ya kampeni.









Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.