MOSHI-KILIMANJARO.
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Majalio Kyara, amelalamikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), hususan Kamati ya Ratiba, kwa kile alichodai ni uvunjaji wa kanuni na ukosefu wa ushirikiano katika masuala ya kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa, Oktoba 17, 2025, mjini Moshi, Kyara alisema chama chake kimekuwa kinapata changamoto kubwa ya mawasiliano na watendaji wa tume, jambo linalosababisha usumbufu katika kufanikisha mikakati na ratiba za kampeni zao.
“Malalamiko yetu ni juu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), hususan Kamati ya Ratiba, tume ilituandikia barua na kutupatia majina pamoja na namba za simu za watu wa kuwasiliana nao lakini changamoto kubwa ni kwamba tumekuwa hatupati ushirikiano mzuri kwenye namba hizo tulizopewa,” alisema Kyara.
Kyara alifafanua kuwa leo walijaribu kuwasiliana na mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Grayson kupitia namba iliyotolewa na tume, lakini kwa zaidi ya saa mbili hawakuweza kuwasiliana naye.
“Tumejaribu kumpigia kwa zaidi ya masaa mawili bila majibu. Baadaye tulipofanikiwa kuwasiliana, majibu tuliyopewa ni kwamba ‘simkai na simu muda wote’. Hii imetukwaza sana kwa sababu ratiba za kampeni zinategemea mawasiliano ya haraka na yenye uhakika,” alisisitiza.
Kyara alisema kwa msaada wa vyombo vya usalama waliweza kuondoka salama, lakini tukio hilo limeonyesha udhaifu mkubwa wa uratibu wa ratiba za kampeni.
"Niwaombe sana wenzetu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi hususani Kamati ya Ratiba, tunapoelekea mwisho wa kipindi chetu cha kampeni, ni kipindi muhimu zaidi changamoto tunazokutana nazo huku ni kubwa tunavumilia, lakini zinatakiwa kushughulikiwa kwa umakini mkubwa,” alisema Kyara.
Alisema hali hiyo inaashiria udhaifu mkubwa katika usimamizi wa ratiba za kampeni za wagombea na inaweza kuathiri haki ya vyama na wagombea kupata fursa sawa za kufanya kampeni kwa mujibu wa sheria na kanuni.
Kyara ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhakikisha inatoa namba mbadala au mawasiliano ya uhakika kwa wagombea wote ili kuwezesha changamoto zinazojitokeza kufikishwa kwa wakati na kushughulikiwa ipasavyo.
“Haiwezekani unapiga simu zaidi ya saa mbili halafu mtu anakuambia hakai na simu muda wote, huu ni udhaifu mkubwa na chanzo cha makwazo haya yote ni mapungufu mengi kwenye upande wa ratiba,” alisema.
Aliongeza kuwa chama chake hakina nia ya kuvuruga mchakato wa uchaguzi, bali kinataka tume ihakikishe usawa na uwazi kwa wagombea wote ili uchaguzi uwe wa haki na huru.
Kwa upande wake Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Moshi vijijini na Vunjo, Lucas Msele, amethibitisha kupokea malalamiko hayo huku, akisema kuwa, kwa mujibu wa ratiba ya INEC, mgombea huyo hakuwa na ratiba ya mkutano katika Jimbo la Vunjo kwa siku ya leo.
"Ni kweli taarifa hizo za malalamiko ya mgombea urais kupitia chama cha SAU nimezipokea lakini kwa masikitiko ni kwamba kwa siku ya leo Oktoba 17,2025 hakuwa na ratiba katika eneo letu, tukiangalia ratiba leo anaonekana ana mikutano eneo la Moshi Mjini"alisema Msele.
Alifafanua kuwa "Wilaya ya Moshi ina majimbo matatu ya Uchaguzi, Jimbo la Moshi Mjini, Moshi Vijijini na Jimbomla Vunjo na kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, mkutano wake leo Oktoba 17,2025 ni Jimbo la Moshi Mjini na kesho Oktoba 18, 2025 anaonekana ana mkutano katika Jimbo la Vunjo eneo la Marangu ndivyo ratiba inasoma."alisema Msele.
Aidha aliongeza kuwa kutokana na Jiografia hakuweza kujua lakini pia alisema huenda kulikuwa na mkanganyiko katika usomaji wa ratiba, na kutoa wito kwa wagombea na viongozi wa vyama vya siasa kuhakikisha wanaisoma na kuielewa vizuri ratiba kabla ya kuelekea maeneo ya mikutano.







