MCHUNGAJI AMTABIRIA USHINDI MGOMBEA UBUNGE MOSHI MJINI

MOSHI-KILIMANJARO.

Mchungaji wa Kanisa la Free Pentecost Tanzania (FPCT) Kiboriloni, Ovena Kowero, amemtangaza mgombea ubunge wa Moshi Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ibrahim Shayo, kuwa ataibuka mshindi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Akizungumza Oktoba 18,2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la Msufini, Kata ya Msaranga, mchungaji Kowero alipewa nafasi ya kumuombea kura mgombea huyo na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Faraji Swai.

Katika maombi yake, mchungaji Kowero alisema amepokea maono kutoka kwa Mungu yakionesha ushindi kwa Shayo, akimueleza kuwa muda wa Mungu kumjibu umefika.

“Sala zako, maombi yako na sadaka zako zimefika mbele za Mungu kama Musa alivyopatiwa fimbo ya kuwaokoa Waisraeli, ndivyo na wewe Mungu amekupa fimbo ya kuwaokoa wananchi wa Moshi Mjini,” alisema mchungaji huyo.










Aidha, mchungaji Kowero aliwaombea pia madiwani wote wa kata 21 za Manispaa ya Moshi Mjini pamoja na madiwani wanane wa viti maalum wa chama hicho, akiwatakia ushindi na hekima ya kuwatumikia wananchi.

“Mkifika kwenye baraza la madiwani, msije kutafuta maslahi yenu binafsi, nendeni kutimiza haja za wananchi watakaowapigia kura na wale wanaowaombea kura,” alisisitiza.

Mkutano huo ulihudhuriwa na mamia ya wakazi wa Kata ya Msaranga, wafuasi wa chama hicho pamoja na viongozi mbalimbali wa CCM ngazi ya wilaya.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.