CHANGAMOTO ZA AFYA, ELIMU, BARABARA ZATAJWA KATA YA MSARANGA

MOSHI-KILIMANJARO.

Mgombea udiwani wa Kata ya Msaranga kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Alhaji Ally Pendo, ameainisha changamoto mbalimbali zinazokabili kata hiyo na kuahidi kuzitatua endapo wananchi watampa ridhaa ya kuwa mwakilishi wao katika uchaguzi mkuu ujao.


Akizungumza Oktoba 18, 2025 kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Mtaa wa Msufini, mgombea huyo alisema sekta za afya, elimu na miundombinu ndizo zenye changamoto kubwa zinazohitaji hatua za haraka.

Katika sekta ya afya, alisema Kituo cha Afya Msandaka kinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa watoa huduma pamoja na matatizo ya mipaka ya eneo hilo.


“Nichagueni ili niweze kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali kuboresha miundombinu ya afya Msandaka, kuhakikisha huduma zinapatikana ipasavyo kwa wananchi,” alisema.

Aliongeza kuwa katika Shule ya Viziwi Msandaka kuna upungufu wa watumishi, hali inayosababisha baadhi ya kazi kufanywa na watu wanaojitolea.

“Nitashauri serikali kuhakikisha wanajitolea hao wanapatiwa ajira rasmi ili kuboresha elimu kwa watoto wenye ulemavu,” alisisitiza.


Aidha, alisema Shule ya Msingi Msandaka inakabiliwa na upungufu wa madawati 50 pamoja na samani za ofisi, huku Shule ya Sekondari Msandaka nayo ikiwa na upungufu kama huo, aliahidi kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha vifaa hivyo vinapatikana kwa wakati.

Kuhusu miundombinu ya barabara, Alhaji Pendo alisema changamoto kubwa ni ukosefu wa vivuko salama na maji ya mvua kuingia kwenye makazi ya watu, akiahidi kushirikiana na mamlaka husika kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo.


“Nikichaguliwa nitahakikisha wahusika wa sekta zote wanawajibika na kuja kushughulikia changamoto hizi kwa vitendo,” alisema.

Pia aligusia suala la uwajibikaji na ushirikishwaji wa wananchi katika shughuli za maendeleo ya kata hiyo, akisisitiza kuwa uongozi wake utakuwa shirikishi na wazi.


Kuhusu mikopo ya serikali kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, alisema ataweka msukumo kuhakikisha fedha hizo zinawafikia walengwa wote kama ilivyokusudiwa.

Aidha, alisema Kata ya Msaranga inayoundwa na mitaa mitatu itaimarishwa kiulinzi na kiusalama kupitia ushirikiano wa karibu kati ya viongozi wa mtaa, jeshi la polisi na wananchi.

 “Tutahakikisha wananchi wanaishi katika mazingira salama, yenye huduma bora na fursa sawa kwa wote,” alisema.
















Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.