LONGUO-MOSHI.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ibrahim Shayo, ameahidi kufadhili miradi ya huduma za kijamii kwa kutumia rasilimali zake binafsi, ikiwa ni pamoja na kununua magari mawili aina ya Costa yatakayotumika bure kwa dharura za wananchi kama misiba, harusi na shughuli nyingine za kijamii.
Shayo alitoa ahadi hiyo Oktoba 14, 2025, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika Mtaa wa Kitandu, Kata ya Longuo B, ambapo alisisitiza dhamira yake ya kugeuza ofisi ya mbunge kuwa chombo cha msaada wa moja kwa moja kwa wananchi.
“Nitanunua magari haya kwa fedha zangu mwenyewe baada ya Oktoba 29 mkishanipa kura za kutosha mtakuwa huru kupiga simu ofisi ya Mbunge mnapokuwa na dharura yoyote magari haya yatakuwa bure kwa wananchi,” alisema Shayo huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Ameongeza kuwa mbali na magari hayo, atanunua ambulance kwa ajili ya wagonjwa na gari ya kubebea maiti ili kupunguza gharama na usumbufu kwa wananchi wenye kipato cha chini wakati wa dharura.
Shayo alisema dhamira yake ni kuhakikisha ofisi ya mbunge inakuwa karibu na wananchi, ikitoa msaada wa kweli unaogusa maisha yao ya kila siku, hususan nyakati za changamoto na uhitaji mkubwa.
Aidha, aliahidi kuweka mwanasheria maalum katika ofisi yake atakayetoa elimu ya kisheria kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Alisema mwanasheria huyo pia atasaidia katika maandalizi ya mikataba na ushauri wa kisheria ili vikundi hivyo viweze kupata mikopo ya halmashauri kwa mujibu wa sheria na taratibu.
“Tutaweka mwanasheria ambaye atakuwa msaada mkubwa kwa vikundi vyote, lengo ni kuhakikisha kila mwananchi anapata fursa ya kujikwamua kiuchumi bila vikwazo vya kisheria,” alieleza Shayo.
Kuhusu watu wenye ulemavu, Shayo alisema hatowalazimisha kujiunga na vikundi ili waweze kupata mikopo, badala yake ataweka utaratibu maalum wa kuwapatia fedha moja kwa moja kama sehemu ya kuimarisha usawa wa kijamii.
“Watu wenye ulemavu nao wanapaswa kupata huduma bila urasimu, nitahakikisha wanapata fedha zao moja kwa moja,” alisisitiza.
Ahadi hizo zimepokelewa kwa shangwe na matumaini makubwa kutoka kwa wakazi wa Longuo B, ambao wameeleza kwamba mpango huo utapunguza kwa kiasi kikubwa gharama za kijamii zinazowakabili.











