MGOMBEA UDIWANI KATA YA KARANGA AAHIDI KUJENGA SHULE MPYA

MOSHI-KILIMANJARO 

Mgombea udiwani wa Kata ya Karanga kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Deogratius Mallya, aliahidi kushughulikia changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda shuleni kwa kuhakikisha ujenzi wa shule mpya ya sekondari ndani ya kata hiyo endapo atachaguliwa kuwa diwani.

Mallya alitoa ahadi hiyo, wakati wa uzinduzi wa kampeni uliofanyika katika kata hiyo na kueleza kuwa shule nyingi zipo mbali na makazi ya wananchi, hali inayowalazimu wanafunzi kutembea hadi kilomita tano kila siku kwenda na kurudi shuleni.

“Hali hii inawaathiri kitaaluma kwani hufika shuleni wakiwa wamechoka na mara nyingine huchelewa, nitahakikisha tunapata suluhisho la kudumu ili watoto wetu wapate elimu katika mazingira rafiki,” alisema Mallya.

Alieleza kuwa shule hiyo itajengwa pembezoni mwa Chuo cha Ufundi Karanga, na itawezesha wanafunzi kupata huduma ya elimu kwa urahisi zaidi bila kutembea umbali mrefu.

Mbali na elimu, Mallya pia aliahidi kuboresha miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami ili kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa kata hiyo.

“Nawaahidi, endapo mtanirudisha madarakani, nitahakikisha barabara zote ndani ya kata zinaunganishwa kwa kiwango cha lami kwa kushirikiana na mamlaka husika,” alisema Mallya.

Ameongeza kuwa wananchi wa Karanga wanahitaji kuona maendeleo ya kweli baada ya miaka 15 ya uongozi wa wapinzani bila mafanikio ya kuridhisha.

“Naomba mnitume tena. Karanga mpya inawezekana,” alisema.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.