FARAJI SWAI: SERIKALI AWAMU YA SITA IMELETA MAENDELEO MAKUBWA MOSHI MJINI

MOSHI-KILIMANJARO

Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi Mjini kimesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeleta mageuzi makubwa ya maendeleo ambayo yameboresha maisha ya wananchi wa Jimbo la Moshi Mjini.

Kauli hiyo imetolewa Oktoba 18,2025 na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Faraji Swai, wakati wa mkutano wa kampeni wa kumnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo, Ibrahim Shayo, uliofanyika katika eneo la Msufini, Kata ya Msaranga.

Swai alisema kuwa kila kata ya jimbo hilo sasa inabeba alama ya miradi ya maendeleo, ikiwemo sekta za afya, elimu na miundombinu ya barabara.

"Kila kata sasa ina alama ya maendeleo tuna shule, zahanati, vituo vya afya na barabara zilizoboreshwa, mfano mzuri ni Kituo kipya cha Afya kilichojengwa Kata ya Shirimatunda,” alisema Swai.

Aidha, alibainisha kuwa miradi ya maji ambayo ilikuwa changamoto kubwa kwa wananchi wa Moshi Mjini, imeboreshwa kwa kiasi kikubwa kupitia miradi iliyosimamiwa na serikali ya Rais Samia.

"Manispaa ya Moshi ina kata 21, zote zina zahanati na nyingine vituo vya afya. Tulikuwa na changamoto ya maji lakini sasa kupitia miradi ya maji ya Rais Samia, adha kubwa ya maji imeondolewa,” aliongeza.

Swai alisema zaidi kuwa serikali imeendelea kuwekeza katika sekta ya afya kwa kiwango kikubwa, akitolea mfano ujenzi wa hospitali mpya ya ghorofa ya wilaya unaoendelea katika Kata ya Ng’ambo mradi ambao utakapokamilika utapunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali za jirani.

“Kwa upendeleo wa kipekee, serikali inatuletea hospitali ya kisasa ya wilaya hapa Moshi Mjini, huu ni ushahidi kuwa serikali ya Awamu ya Sita inafanya kazi,” alisema.

Kauli hiyo imeungwa mkono na viongozi na wanachama wa chama hicho waliokuwa wamekusanyika katika mkutano huo, wakisisitiza kuwa maendeleo hayo ni matokeo ya uongozi makini na sera thabiti za CCM.












Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.