CCM KALOLENI WAANZA KAMPENI ZA NYUMBA KWA NYUMBA KUMUOMBEA KURA RAIS SAMIA

KALOLENI-MOSHI.

Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kaloleni, Manispaa ya Moshi, kimeanza rasmi kampeni za kuomba kura kwa wananchi kwa kutembelea nyumba kwa nyumba na mtaa kwa mtaa, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kumuombea kura mgombea urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, mgombea ubunge Ibrahim Shayo, (Ibra Line) na mgombea udiwani wa kata hiyo Nasibu Mariki.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hizo, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kaloleni, Joshua Othiambo Kojo, alisema wameamua kutumia mbinu hiyo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, hususan wazee na wagonjwa ambao hawawezi kuhudhuria mikutano ya hadhara ya kampeni.

:Tumeamua kufanya kampeni hii ya nyumba kwa nyumba na mtaa kwa mtaa kwa ajili ya kuwafikia wazee na wagonjwa ambao wako kitandani, tumewafikia na wametuelewa vizuri,” alisema Kojo.

Kojo aliongeza kuwa kampeni hizo zitaendelea hadi Oktoba 29, mwaka huu, huku akitoa wito kwa wananchi wa kata hiyo kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa wagombea wote wa CCM.

Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kata ya Kaloleni Nasibu Mariki, alisema kampeni za nyumba kwa nyumba ni utaratibu wa chama unaolenga kuhakikisha ujumbe wa chama unawafikia watu wote bila kujali mazingira yao.

"Sio watu wote wanaohudhuria mikutano ya hadhara, wengine wanakuwa kwenye shughuli zao au wagonjwa kwa kwenda nyumba kwa nyumba, tumefanikiwa kuwafikia watu wengi zaidi,” alisema Mariki.

Aliongeza kuwa katika ziara hiyo wamebaini wananchi wengi hawakuwa wanajua ratiba za mikutano ya kampeni, jambo ambalo limewasaidia kutoa elimu na hamasa ya kushiriki uchaguzi.

Kata ya Kaloleni inajumuisha jumla ya wanachama 6,526 waliojiandikisha kwenye Daftari la Mpiga Kura, ambapo Mariki alisema ana matumaini kuwa Rais Samia Suluhu Hassan atapata kura zaidi ya asilimia 95, sambamba na ushindi kwa mbunge na Diwani.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.