CCM MOSHI MJINI YAKABIDHI PIKIPIKI 21 KWA MADIWANI KUSAKA KURA ZA RAIS SAMIA

MOSHI-KILIMANJARO.

Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi Mjini kimekabidhi pikipiki 21 kwa madiwani wateule wa chama hicho ili kusaidia kampeni za kumtafutia kura mgombea urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao.


Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika viwanja vya ofisi ya CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Katibu wa CCM wilayani humo, Amos Shimba, alisema kuwa pikipiki hizo ni zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk. Samia Suluhu Hassan, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


“Jimbo la Moshi Mjini lina kata 21, na leo nimewakabidhi madiwani wetu pikipiki hizi kwa ajili ya kwenda kusaka kura za mgombea urais Dk. Samia Suluhu Hassan, nyumba kwa nyumba, mtaa kwa mtaa,” alisema Shimba.

Shimba alisisitiza kuwa matumizi ya pikipiki hizo yanapaswa kuwa ya kisiasa tu, si kwa shughuli binafsi kama bodaboda.

Kwa upande wake, Mstahiki Meya Mstaafu na mgombea udiwani wa Kata ya Njoro, Alhaji Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, aliishukuru serikali ya CCM kwa msaada huo na kuahidi kuitumia pikipiki hiyo kufanikisha kampeni za chama.

“Nipende kukuhakikishia kwamba chombo hiki nitakitumia kwa malengo yaliyokusudiwa na chama changu, kwani kitanirahisishia kuwafikia wananchi wengi katika kutafuta kura za Rais na Mbunge,” alisema Kidumo.


Naye mgombea udiwani wa Kata ya Kiusa, Khalid Shekoloa, alisema kuwa kata hiyo ina wapiga kura 5,338 waliojiandikisha, na kutokana na kazi kubwa ya maendeleo aliyowahi kufanya, ana matumaini makubwa ya kuungwa mkono na wananchi.

“Tumeletewa fedha nyingi za miradi ya maendeleo hapa Kiusa, hivyo naamini wakazi wa kata hii wataniamini na kumpa kura nyingi Rais Samia Suluhu Hassan,” alisema Shekoloa.

Makabidhiano hayo ni sehemu ya jitihada za chama hicho kuhakikisha kinaimarisha mtandao wa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu, kwa kuwapa madiwani uwezo wa kuwafikia wananchi moja kwa moja katika maeneo yao.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.