MGOMBEA UDIWANI KATA YA MIEMBENI HARUNA MUSHI "INASIKITISHA SHULE ZA UMMA KUKOSA VYOO"


MOSHI-KILIMANJARO

Shule tatu za umma  zilizoko katika Kata ya Miembeni halmashauri ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro,  zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa matundu ya vyoo, hali inayowalazimu walimu na wanafunzi kuchangia vyoo vichache vilivyopo, na hivyo kuhatarisha afya na ustawi wa wanafunzi.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika Oktoba 13, 2025, katika eneo la shule ya Sekondari J.K. Nyerere, mgombea udiwani wa Kata ya Miembeni kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Haruna Ally Mushi, alieleza kuwa zaidi ya matundu 50 ya vyoo yanahitajika ili kukidhi mahitaji ya shule hizo.

"Naombeni mnichague Oktoba 29 mwaka huu niende kwenye Baraza la Madiwani ili niweze kuisukuma serikali itenge fedha za ujenzi wa vyoo katika shule ya msingi mjimpyia, Miembeni na Shule ya Sekondari J.K. Nyerere," alisema Mushi.

Aliongeza kuwa iwapo atapewa ridhaa ya kuwatumikia wananchi wa Kata ya Miembeni, atahakikisha suala hilo linapewa kipaumbele katika vikao vya halmashauri, kwa kushirikiana na mamlaka husika.

Mbali na changamoto ya vyoo, Mushi pia alieleza kuwa barabara za ndani ya kata hiyo zimekuwa kero kubwa kwa wananchi, na kwamba atapigania kutafutwa kwa suluhisho la kudumu.

"Ninajua barabara za ndani ni kilio cha muda mrefu, lakini nami nipo tayari kushirikiana na uongozi kuhakikisha tunapata barabara bora zinazopitika wakati wote wa mwaka," alisisitiza.

Katika mkutano huo, Mushi pia aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta maendeleo katika kata hiyo.


Alieleza kuwa katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, serikali imeleta zaidi ya shilingi milioni 44.5 katika kata ya Miembeni.

Kati ya fedha hizo, shilingi milioni 4.5 zilitumika kujenga ukuta wa shule ya Sekondari J.K. Nyerere, huku shilingi milioni 40 zikiidhinishwa kwa ajili ya ukarabati wa maabara mbili katika shule hiyo.














Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.