MOSHI-KILIMANJAO.
Baadhi ya Vijana wa Moshi Mjini wametoa ushuhuda mzito kuhusu mchango mkubwa wa mgombea ubunge wa jimbo hilo, Ibrahim Shayo maarufu kama (Ibra-Line), ambaye amekuwa msaada mkubwa kwa jamii hasa pale wanapompelekea changamoto za moja kwa moja.
Mkazi wa Kata ya Pasua, Hassan Yusuph Mnzava, ameyasema hayo Oktoba 20, mwaka huu katika mkutano wa kampeni uliofanyika Eneo la Stendi ya Haice Pasua, Mtaa wa Majengo Mapya.
Amesema mgombea huyo amekuwa kimbilio kwa makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo vijana, wazee, wajane, watu wenye ulemavu na wengine walioko katika hali ngumu za maisha.
“Changamoto za kila siku tunazozipata, mgombea huyu amekuwa msaada mkubwa na daima anasikiliza matatizo yetu na kutafuta njia za kutusaidia,” alisema Mnzava.
Kwa mujibu wa vijana hao walisema kuwa Oktoba 29, mwaka huu watamchagua mgombea huyu kutokana na moyo wake wa kujitolea na huduma kubwa aliwapa kabla hata hajakuwa mbunge rasmi.
"Ibra-Line ana moyo wa kweli wa kusaidia jamii na amekuwa msaada wa kipekee,” alisema Mnzava ambaye ni mmoja wa vijana.
Mnzava ambaye ni mmoja wa vijana wqlionufaika kupata ajira kupitia kampuni ya mgombea huyo ambapo amesema anapokea mshahara wa Sh 900,000 kila mwezi.
"Kama si kwa moyo wake wa kujitolea, huenda nisingekuwa na ajira hii,” aliongeza Mnzava.
Aidha,Mnzava alieleza jinsi mgombea huyo alivyomchukua mtoto wa aliyekuwa Katibu Mwenezi wa CCM Kata ya Pasua, aliyefariki na kumsaidia kusoma hadi kumaliza kidato cha sita, mtoto huyo kwa sasa anafanya kazi katika Jeshi la Polisi, kitengo cha kutuliza ghasia (FFU).
Mnzava alisisitiza kuwa hakuna familia au jamaa yeyote aliyekosa kunufaika na misaada ya kibinadamu inayotolewa na mgombea huyo wakati wa changamoto mbalimbali.
"Kwa niaba ya vijana wenzangu tunakuahidi mgombea ubunge, tutajitokeza kwa wingi wingi kumpigia kura mgombea urais wa CCM Dk Samia Suluhu Hassan, wewe mwenyewe Ibrahim Shayo, na diwani wetu Barreh Ally Farrah na hii ni njia ya kukushukuru ili uweze kuendelea kutetea maslahi wananchi wa Moshi Mjini bungeni.








