MGOMBEA UDIWANI PASUA AHAIDI KUWAUNGANISHA VIJANA NA FURSA ZA AJIRA

MOSHI-KILIMANJARO.

Mgombea Udiwani wa Kata ya Pasua, Barreh Ally Farrah, ameahidi kutumia mitandao na uhusiano alionao ili kuwaunganisha vijana na fursa mbalimbali za ajira katika sekta binafsi endapo atachaguliwa kuwa Diwani.

Akizungumza Oktoba katika mkutano wa kampeni uliofanyika Mtaa wa Majengo Mapya, eneo la Stendi ya Pasua, Barreh alisema vijana wengi waliomaliza elimu ya juu na vyuo vya kati bado hawajapata ajira rasmi, jambo linalokwamisha maendeleo yao ya kiuchumi.

“Vijana wengi wana sifa na elimu nzuri lakini hawana ajira, nikipewa nafasi ya kuwa Diwani, nitaitumia vizuri mitandao yangu na taasisi binafsi kuwaleta karibu na waajiri ili wapate kazi na kuimarisha uchumi wao,” alisema Barreh.

Ameongeza kuwa Kata ya Pasua ina viwanda na taasisi nyingi binafsi, hivyo zipo fursa kubwa za vijana kupata ajira endapo kutakuwa na kiongozi mwenye maono na ushawishi wa kuwaunganisha na sekta hizo.

Barreh alisema vipaumbele vyake vitatu ni Mahusiano, Maono na Maendeleo.

Katika kipengele cha Maono, ameahidi kupigania ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara katika kata hiyo, ikiwemo barabara ya Mwisho wa Hiace hadi TEXS na ile ya Soko hadi Reli, ambazo alisema zinahitaji kuwekwa lami, taa za barabarani na mitaro ya maji ya mvua.

Kuhusu Maendeleo; ameahidi kuhakikisha wananchi wanapata fursa za kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri, pamoja na kuhamasisha miradi mbalimbali ya kijamii itakayowanufaisha wananchi wote wa kata hiyo.

Aidha, Barreh amesema atahakikisha anasimamia kwa vitendo Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030, ambayo ameielezea kama mkataba kati ya wapiga kura na viongozi wanaochaguliwa.

"Nitasimamia kikamilifu Ilani ya CCM, yale yote yaliyoandikwa ndani ya ilani hiyo nitayatekeleza kwa vitendo kwa ajili ya wananchi wa Pasua,” alisisitiza.





Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.