MSARANGA-MOSHI.
Mgombea udiwani wa Kata ya Msaranga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Alhaj Ally Pendo, amesema kuwa wapo baadhi ya wazee katika kata hiyo ambao hawajawahi kuingizwa kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) licha ya kuwa na uhitaji mkubwa wa msaada huo.
Alhaj Pendo aliyasema hayo wakati wa mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika katika Mtaa wa Msufini, na kuhudhuriwa na mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, pamoja na viongozi mbalimbali wa CCM ngazi ya wilaya wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Faraji Swai.
“Nipeni ridhaa niwe diwani wenu ili niweze kuwawakilisha kwenye baraza na kuwapigania hawa wazee waingizwe kwenye mpango wa TASAF. Hawa ni watu wanaohitaji sana msaada huu wa serikali,” alisema Pendo.
Mbali na hilo, mgombea huyo alitaja changamoto ya miundombinu ya barabara katika kata hiyo, akiahidi kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha barabara zinakarabatiwa ili kurahisisha usafiri na kuinua uchumi wa wakazi.
“Barabara zikikarabatiwa itarahisisha kusafirisha bidhaa, kuongeza fursa za kibiashara na kuinua kipato cha wananchi,” aliongeza.








