SHIO AWAAHIDI WANANCHI WA KATA YA SHIRIMATUNDA KITUO CHA POLISI

MOSHI-KILIMANJARO.

Mgombea udiwani wa Kata ya Shirimatunda, halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Francis Shio, ameahidi kuanzisha kituo cha polisi kitakachofanya kazi saa 24 endapo atachaguliwa tena katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Akihutubia wakazi wa kata hiyo katika mkutano wa kampeni uliofanyika Oktoba 22, 2025 katika eneo la Ostabay, mtaa wa Kigongoni, Shio alisema Kata ya Shirimatunda kwa muda mrefu imekuwa haina kituo cha polisi hali inayowapa changamoto wananchi katika masuala ya usalama.

“Kata ya Shirimatunda haina kituo cha polisi, tunahitaji kituo kitakachofanya kazi saa 24 ili kuhakikisha usalama wa wananchi wetu unalindwa wakati wote,” alisema Shio.

Shio, ambaye ameongoza kata hiyo kwa miaka 10, alisema katika kipindi chake kijacho cha miaka mitano, atapigania mambo mawili ya msingi: kuimarishwa kwa barabara na kuanzishwa kwa kituo cha polisi cha kudumu.

Alisema baadhi ya barabara katika kata hiyo zimefunguliwa na kuimarishwa, lakini bado kuna barabara tano ambazo hazipitiki kabisa, zikiwemo, barabara ya Kwandigao, barabara ya Kradeda, barabara ya Haice hadi Mjoshoni, barabara ya Mmasi na barabara ya Kwamrefu.

“Mkinipa kura Oktoba 29, ndani ya mwezi mmoja nitaanza kuchukua hatua za kuhakikisha barabara hizi zinapitika na zinawasaidia wananchi katika shughuli zao za kila siku,” aliahidi.

Katika mkutano huo, Shio pia alieleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, akisema kuwa serikali imetoa shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya kuipandisha hadhi zahanati ya kata hiyo kuwa kituo cha afya.

Alisema kituo hicho cha afya sasa kina jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la mama na mtoto, pamoja na majengo yote yanayohitajika kwa huduma za afya kwa wananchi.

Kwa upande wa elimu, Shio alitaja mafanikio yaliyopatikana kuwa ni pamoja na ujenzi wa shule mpya ya sekondari yenye hosteli ya wasichana 220, pamoja na shule mbili mpya za msingi.

Aliongeza kuwa shule ya Tumaini imejengwa kwa nguvu za wafadhili na inatoa mchango mkubwa kwa elimu ya watoto wa kata hiyo.

Akigusia sekta ya ardhi, alisema kata hiyo haikuwa na mpango wa urasimishaji wa makazi, lakini kupitia ushirikiano na wananchi, wamefanikiwa kuhakikisha watu wanamiliki ardhi kwa hati halali.

“Kata ya Shirimatunda haikuwa na mpango kazi wa urasimishaji wa makazi, lakini leo hii, wananchi wamepimiwa na wanamiliki ardhi zao kihalali,” alisema.

Aliongeza kuwa katika maeneo ya Kigongoni na Bonite Viwandani, wananchi wamepimiwa viwanja, baadhi wamepata hati miliki, na wengine wanaendelea kufuatilia taratibu.

Shio alihitimisha hotuba yake kwa kuwaomba wananchi waliopo kwenye daftari la wapiga kura zaidi ya 4,500, katika kata hiyo , kumpigia kura mgombea urais Dk Samia Suluhu Hassan, mbunge Ibrahim Shayo na yeye kwa nafasi ya udiwani ili aweze kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chake cha awali.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.