MGOMBEA UDIWANI SOWETO AAINISHA CHANGAMOTO ZA MIUNDOMBINU YA BARABARA, MASOKO

MOSHI-KILIMANJARO.

Mgombea udiwani wa Kata ya Soweto kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul George Maile, ameainisha changamoto mbalimbali zinazowakabili wakazi wa kata hiyo, ikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara na masoko, na kuahidi kuzitafutia ufumbuzi endapo ataaminiwa na wananchi katika uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumza Oktoba 19,2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la Stendi ya Bajaj, Kata ya Soweto, Maile alisema changamoto kubwa inayowakabili wananchi ni hali mbaya ya barabara ambazo hazipitiki hususan kipindi cha mvua.

Alizitaja barabara zinazohitaji matengenezo kuwa ni Barabara ya Bima hadi Mawazo, Mzambarauni, Usalama hadi Makanyaga, na Barabara ya Mviringo. Nyingine ni Ngorongoro hadi Msikitini, Sabasaba ndani, Magereza, Tupendane hadi Chekanao, pamoja na Barabara ya Scorpion hadi Mama Clementina.

“Barabara hizi hazipitiki kabisa wakati wa mvua, zipo zinazohitaji kuwekwa lami na zingine kujengewa mifereji ya maji ya mvua ili yasipenye kwenye makazi ya watu,” alisema Maile.

Aliahidi kwamba endapo wananchi watampa ridhaa Oktoba 29, 2025, atashirikiana na Mbunge na Serikali ya CCM kuziombea fedha barabara hizo ziweze kutengenezwa.

Akizungumzia sekta ya masoko, Maile alisema Kata ya Soweto ina masoko mawili muhimu, Soko la Mawazo na Soko la Mitumba la Memorial, ambayo miundombinu yake imechakaa na inahitaji maboresho ya haraka.

Alisema Soko la Mawazo linakabiliwa na changamoto ya miundombinu chakavu, hali inayosababisha wafanyabiashara kufanya kazi katika mazingira magumu, hasa kipindi cha masika.

“Wafanyabiashara wa soko hili wanafanya kazi katika mazingira yasiyo rafiki, nikichaguliwa nitaomba fedha kwenye baraza ili soko liboreshwe, kuwekwa taa na mazingira mazuri yatakayowawezesha kufanya biashara hata usiku,” alisema.

Kwa upande wa Soko la Memorial, Maile alisema changamoto kubwa ni ubovu wa barabara unaosababisha tope na kuzorotesha shughuli za kibiashara wakati wa mvua, pamoja na kukosekana kwa vyoo vya umma.

“Wafanyabiashara wanalipa kodi na ushuru lakini mazingira ya kufanya biashara si rafiki, nikipewa ridhaa nitapambania maboresho ya soko hili kupitia baraza la madiwani,” aliongeza.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, aliwaomba wananchi wamchague ili aweze kupeleka sauti yao bungeni na kupigania kuongezwa bajeti ya TARURA kwa ajili ya kuboresha barabara.

Shayo alisema kwa sasa TARURA Moshi Mjini inatengewa shilingi bilioni 4.6, kutoka bilioni 2.3 zilizokuwa awali, kiasi ambacho bado hakitoshi kukidhi uhitaji mkubwa wa miundombinu ya barabara.

Aliongeza kuwa anazitambua changamoto zilizoko katika Soko la Memorial ikiwemo ubovu wa barabara na ukosefu wa vyoo, na kuahidi kupigania maboresho yake endapo atachaguliwa.













Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.