MOSHI-KILIMANJARO.
Mkazi wa Kata ya Soweto, Bi. Jamila Shaban Kumuaya, amepanda jukwaani na kumshukuru mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, kwa kumsaidia kulipia gharama za matibabu ya baba yake mzazi.
Jamila alitoa shukrani hizo Oktoba 19, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la Stendi ya Bajaj, Kata ya Soweto, ambapo alieleza namna mgombea huyo alivyojitokeza kumsaidia katika kipindi kigumu.
Amesema mwaka 2020 baba yake mzazi alilazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) kutokana na tatizo la ini lililosababisha tumbo kujaa, na alihitaji kufanyiwa upasuaji wa haraka.
“Gharama za upasuaji zilikuwa shilingi milioni 1.5, kiasi ambacho familia yetu haikuweza kukimudu, niliamua kwenda kumuomba msaada Bwana Ibrahim Shayo, naye bila kusita alitoa fedha hizo,” amesema Jamila.
Ameongeza kuwa kutokana na msaada huo, waliweza kulipia gharama za matibabu na baba yake alifanyiwa upasuaji kisha kuruhusiwa kurudi nyumbani akiwa na afya njema.
“Ninamshukuru sana kwa moyo wake wa kujitolea kusaidia watu wasio na uwezo. Mungu azidi kumbariki kwa wema wake,” amesema kwa hisia Jamila mbele ya umati wa wananchi waliohudhuria mkutano huo wa kampeni.







