TAMASHA LA KAHAWA LATAJWA KUWA JUKWAA MUHIMU LA ELIMU NA FURSA ZA KIUCHUMI

MOSHI-KILIMANJARO.

Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Tanzania, Dk. Benson Ndiege, amesema kuwa tamasha la Kahawa ni jukwaa muhimu linalotoa elimu kuhusu ubunifu, fursa za kiuchumi na kuwaunganisha wadau wa sekta ya kahawa nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tamasha hilo uliofanyika Oktoba 3, 2025, mjini Moshi, Dk. Ndiege alisisitiza umuhimu wa wadau kushiriki kikamilifu katika tamasha hilo ambalo lina lengo la kuhamasisha, kuinua na kuongeza thamani ya zao la kahawa , ambalo ni moja ya mazao ya kimkakati ya kiuchumi nchini Tanzania.

“Ni fursa adhimu kwa wakulima, wasindikaji, wanunuzi na wadau wengine wa kahawa kukutana, kubadilishana uzoefu, kujifunza na kujenga ushirikiano wa kibiashara utakaosaidia kuendeleza tasnia ya kahawa nchini,” alisema Dk. Ndiege.

Aidha, alihimiza wananchi na wadau kujitokeza kwa wingi kushiriki katika tamasha hilo la siku tatu, linalofanyika katika eneo la kiwanda cha kukoboa kahawa cha Tanganyika Coffee Curing Company Ltd (TCCCo), mjini Moshi, kwa lengo la kunufaika na mafunzo mbalimbali yatakayotolewa.

Tamasha hilo la Kahawa Festival 2025 ambalo linafanyika kwa siku tatu mfululizo, limeingia siku yake ya pili leo Oktoba 4, 2025, likishuhudia ushiriki mkubwa wa wageni kutoka sekta mbalimbali, tamasha linatarajiwa kufikia tamati Oktoba 5, 2025.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.