MOSHI-KILIMANJARO.
Chama Kikuu cha Ushirika cha Kagera (KCU-1990) Ltd kimesema kuwa katika msimu wa kilimo wa 2025/2026, kinatarajia kusambaza miche bora ya kahawa 300,000 kwa wakulima wa kilimo hai, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwa ajili ya soko la nje.
Hayo yamesemwa Oktoba 3,2025, mjini Moshi na Mwenyekiti wa Bodi ya (KCU 1990) Ltd, Ressy Mashulano, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Sita ya Kahawa Festival 2025, yanayofanyika katika Ukumbi wa Kiwanda cha Kukoboa Kahawa cha Tanganyika TCCCO. Kilichopo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Mashulano alisema kuwa miche hiyo itatolewa kwa wakulima wanaotoka katika vyama 32 vinavyoshiriki katika kilimo hai, ambayo kwa sasa inazidi kupata soko kubwa kwenye nchi za Ulaya.
“Mpango huu unalenga kuunga mkono jitihada za serikali katika kufikia uzalishaji wa zaidi ya tani 300,000 za kahawa ifikapo mwaka 2030,” alisema.
Alisema kuwa katika kipindi cha kati ya mwaka 2024 hadi 2025, (KCU-1990) Ltd, ilisambaza miche 200,000 ya kahawa kwa wakulima wa kilimo hai, na kufuatilia maendeleo yake kupitia maafisa ugani 31 ambao wamewaajili, huku alieleza kuwa matokeo ya uwekezaji huo yanatarajiwa kuanza kuonekana baada ya miaka mitatu.
Kwa mujibu wa Mashulano, alisema kahawa ya kilimo hai inayozalishwa kupitia usimamizi wa KCU-1990 Ltd, huuzwa nje ya nchi, hususan katika masoko ya Ulaya, na hivyo kusaidia kuongeza mapato ya fedha za kigeni kwa taifa.
"Katika msimu wa 2024/2025 tuliuza tani 1,138 za kahawa, na msimu huu wa 2025/2026 tunatarajia kukusanya zaidi ya tani 1,700,” alifafanua.
Kuhusu upatikanaji wa miche bora, Mashulano alisema kuwa kati ya vyama 142 vya msingi vilivyo chini ya KCU-1990 Ltd, vyama 110 hupokea miche kutoka katika vitalu vinavyosimamiwa na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), ambapo KCU-1990 Ltd, imetoa maeneo matatu kwa TCB kwa ajili ya uzalishaji wa miche hiyo, yakiwemo mashamba mawili Bukoba na moja Mleba, ambapo takribani miche milioni 2 huzalishwa kila mwaka.
Mbali na shughuli za uzalishaji na biashara ya kahawa, KCU-1990 Ltd, pia imewekeza kwenye miradi mingine ya maendeleo ya kiuchumi kwa ajili ya kuongeza mapato ya chama hicho.
"Tumejenga ukumbi wa kisasa wa mikutano wenye thamani ya shilingi milioni 900, nyumba za kupangisha, na tunamiliki maduka 47 yaliyoko Bukoba mjini,” alisema.
Aliongeza kuwa kwa sasa KCU-1990 Ltd, inajenga hoteli ya kisasa ya nyota tano ambayo gharama yake hadi kukamilika inakadiriwa kufikia shilingi bilioni 7.
Aidha Mashulano alitoa wito kwa wakulima, kuendelea kuzingatia kilimo hai, akieleza kuwa mbali na kuwa chanzo cha kipato, kilimo hicho pia kinasaidia kulinda mazingira na kuhifadhi afya za binadamu.












