MOSHI-KILIMANJARO.
Wakulima wa kahawa nchini wamehimizwa kutumia miche bora inayozalishwa na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) ili kuongeza uzalishaji na tija katika sekta hiyo muhimu ya kilimo.
Wito huo umetolewa jana na Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Tanzania, Dk. Benson Ndiege, wakati wa ufunguzi wa Maonyesho ya Msimu wa Sita ya Kahawa (Coffee Festival-2025), yanayofanyika katika Kiwanda cha Kukoboa Kahawa cha Tanganyika TCCCO, kilichopo mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Dk. Ndiege alisema serikali kupitia Bodi ya Kahawa imekuwa ikitoa miche bora ya kahawa bure kwa wakulima, na kwa mwaka huu wa fedha inatarajia kugawa miche milioni 20, hivyo ni muhimu wakulima kuitumia fursa hiyo ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo lenye thamani kubwa kiuchumi.
"Serikali inatambua umuhimu wa sekta ya kilimo kwa kuwa zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wanajihusisha nayo, hii ndiyo sababu bajeti ya kilimo imeendelea kuongezeka kila mwaka, ikiwa ni pamoja na ruzuku ya pembejeo zenye bei nafuu zinazowasaidia wakulima wengi," alisema Dk. Ndiege.
Akizungumzia mafanikio ya sekta ya kahawa, Dk. Ndiege alisema uzalishaji wa kahawa katika Kanda ya Kaskazini umeongezeka kutoka tani 8,000 hadi kufikia tani 12,000 katika kipindi cha miaka miwili, sawa na ongezeko la asilimia 37. Katika ongezeko hilo, mkoa wa Kilimanjaro unachangia tani 3,000.
"Uzalishaji huu umeongezeka kwa kiasi kikubwa, na mkoa wa Kilimanjaro umeendelea kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa kahawa nchini," aliongeza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Prof. Auleria Kamuzora, alisema bodi hiyo imeshuhudia mafanikio makubwa kwa wakulima wa kahawa, ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa maisha yao.
"Tunaona wakulima wakijenga nyumba bora, wakinunua vyombo vya usafiri, na uchumi wao kwa ujumla ukiimarika kutokana na ongezeko la bei ya kahawa," alisema Prof. Kamuzora.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Primus Kimaryo, aliwahamasisha Watanzania kuendelea kutumia kahawa ya ndani ili kukuza uchumi wa nchi na wa wakulima.
"Unapokunywa kahawa ya ndani, unachangia kukuza uchumi wa mkulima, unaongeza ajira na kipato kwa Watanzania, na pia unalinda afya yako," alisema Kimaryo.









