POSTA KUFUNGUA MADUKA YA KUBADILISHA FEDHA ZA KIGENI KATIKA MIKOA YENYE UZALISHAJI WA KAHAWA


MOSHI-KILIMANJARO.

Shirika la Posta Tanzania limejipanga kimkakati kufungua maduka ya kubadilisha fedha za kigeni katika mikoa yote inayolima kahawa nchini, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kuimarisha mnyororo wa thamani wa zao hilo.

Hayo yamesemwa jana na Meneja wa Shirika la Posta mkoa wa Kilimanjaro, Abubakar Athuman Jangufua, wakati wa ufunguzi wa maonyesho ya Sita ya Kahawa (Kahawa Festival 2025) yanayofanyika kwa siku tatu katika Kiwanda cha Kukoboa Kahawa cha Tanganyika TCCCO, mjini Moshi.

Jangufua alisema hatua hiyo inalenga kuwasaidia wakulima, wanunuzi na wadau wengine wa zao la kahawa kuepuka changamoto za kubadilisha fedha za kigeni, hasa katika maeneo ya uzalishaji ambako huduma hizo zimekuwa adimu.

“Mnununuzi au mkulima anapotaka kubadilisha fedha au kununua kahawa, sisi Posta tumeimarika katika eneo hilo, tunalenga kuiwezesha sekta ya kahawa isiwe na mkwamo wowote,” alisema Jangufua.

Alifafanua kuwa, pamoja na huduma hiyo ya ubadilishaji wa fedha, Posta pia imeendelea kutoa mchango mkubwa katika usafirishaji wa kahawa kutoka mikoa ya Kusini hadi Kaskazini na Dar es Salaam, kupitia magari yake ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 3.5 hadi 30.

"Tunayo magari ya aina mbalimbali yanayotumika kusafirisha kahawa kwa usalama na kwa wakati, jambo ambalo limewasaidia wakulima na wanunuzi wakubwa kuhakikisha mazao yao yanafika mahali yanapotakiwa kufikishwa,” aliongeza.

Aidha, alieleza kuwa Posta kupitia huduma ya EMS, imekuwa ikisaidia usafirishaji wa mizigo, nyaraka, na sampuli za kahawa ndani na nje ya nchi, kwa njia rahisi, salama na ya uhakika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Prof. Auleria Kamuzora, aliipongeza Posta kwa kushiriki katika maonyesho hayo, akisema kuwa ushiriki huo ni ishara ya namna sekta mbalimbali zinavyoendelea kuona fursa katika zao hilo.

"Niupongeze sana uongozi wa Shirika la Posta kwa kushiriki katika Kahawa Festival 2025, tangu kuanzishwa kwa maonyesho haya, idadi ya washiriki imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka, jambo linaloonyesha kuwa maonyesho haya yanazidi kukua na kuhamasisha sekta ya kahawa nchini,” alisema Prof. Kamuzora.

Maonyesho ya Kahawa Festival hufanyika kila mwaka yakikusanya wadau mbalimbali wa kahawa wakiwemo wakulima, wanunuzi, wasindikaji na taasisi za kifedha na usafirishaji, kwa lengo la kukuza sekta hiyo muhimu katika uchumi wa taifa.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.