NJIAPANDA-HIMO.
Mgombea udiwani wa Kata ya Njiapanda, halmashauri ya Wilaya ya Moshi John Mapato Meela, ameibua changamoto ya muda mrefu inayowakabili wakazi wa kata hiyo, ambayo ni ukosefu wa eneo rasmi la makaburi kwa ajili ya maziko ya wapendwa wao.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Oktoba 2, 2025, katika eneo la Stand ya Juu, Meela alisema kuwa kwa sasa wananchi hulazimika kuzika majumbani kwao kwa kificho, jambo linalokiuka sheria na kuleta athari za kijamii na kiafya.
"Kata ya Njiapanda haina eneo la makaburi, wananchi wanapopoteza ndugu, hulazimika kuwazika kwenye maeneo yao binafsi, licha ya kwamba sheria hairuhusu. Nikichaguliwa kuwa diwani, nitashirikiana na Mbunge wetu, Enock Zadock Koola, kuhakikisha tunatafuta na kununua eneo la angalau heka tano kwa ajili ya makaburi ya jamii,” alisema Meela.
Alieleza kuwa tayari Kata ya Njiapanda imeshatangazwa kuwa Mamlaka ya mji mdogo, hivyo ni muhimu kwa viongozi kuhakikisha miundombinu na huduma za msingi, ikiwemo eneo la makaburi, zinapatikana kwa wananchi.
Mbali na suala hilo, Meela alitaja changamoto ya miundombinu ya barabara za ndani, akisema nyingi hazipitiki nyakati za mvua, jambo linalozorotesha maendeleo na huduma za kijamii.
"Tutahakikisha tunaingiza katapila kwa ajili ya kufungua barabara zote na kuziweka kwenye kiwango cha changarawe ili ziweze kupitika misimu yote,” aliongeza.
Aidha mgombea udiwani huyo alisema changamoto nyingine kubwa aliyoitaja ni ukosefu wa soko la mazao ya mboga mboga, hali inayowalazimisha wajasiriamali kufanya biashara kandokando mwa barabara kuu, jambo ambalo ni hatari kwa usalama wao na wa watumiaji wa barabara.
“Katika kipindi changu cha miaka mitano nikiwa diwani, nitaweka mkazo katika kujenga soko la kisasa kwa kushirikiana na halmashauri na Serikali ya CCM ili wajasiriamali wafanye biashara katika mazingira salama,” alisema.
Meela pia aligusia tatizo la uhalifu, akiahidi kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi (sungusungu) ili kudhibiti vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na baadhi ya vijana wanaojihusisha na wizi.
Kwa upande wa sekta ya kilimo, Meela alisema Kata ya Njiapanda ina mifereji ya umwagiliaji lakini miundombinu hiyo haijaboreshwa kwa muda mrefu, ameahidi kushirikiana na wataalamu wa Tume ya umwagiliaji ili kuiimarisha kwa manufaa ya wakulima.
“Tutafanya maboresho ya mifereji ya umwagiliaji ili kuhakikisha wakulima wetu wananufaika na kilimo cha kisasa na kuongeza tija,” alisema.
Mgombea huyo amewaomba wananchi wa Kata ya Njiapanda kumpa ridhaa ya kuwa diwani wao ili aweze kushirikiana nao kutatua changamoto hizo kwa vitendo.













