DK. SAMIA AAHIDI UJENZI WA CHUO CHA BIASHARA WILAYANI HAI


MOSHI-KILIMANJARO.

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuwa endapo atachaguliwa kuunda serikali baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, atahakikisha Serikali yake inajenga tawi la Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) katika Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza jana kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika Viwanja vya Mashujaa mjini Moshi, Dkt. Samia alisema lengo la ujenzi huo ni kupanua fursa za elimu ya juu, kuongeza ujuzi kwa vijana na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika mkoa huo.

“Katika kutekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya kuendeleza elimu nchini, tutajenga tawi la Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) wilayani Hai ili kuinua wananchi wa mkoa huu kitaaluma, hususan katika elimu ya biashara,” alisema Dkt. Samia.


Tawi hilo linatarajiwa kujengwa katika Kijiji cha Shiri Njoro, Kata ya Mnadani, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali kupanua wigo wa vyuo vya elimu ya juu na mafunzo ya ufundi (VETA) katika kila wilaya nchini.


Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Prof. Edda Tandi Lwoga, alisema uamuzi wa kujenga tawi hilo kwa mara ya kwanza katika Ukanda wa Kaskazini utaongeza upatikanaji wa elimu ya biashara kwa vijana wengi nchini.

"Chuo chetu kwa sasa kina matawi manne Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya na Mwanza. Tawi jipya la Kilimanjaro litapanua huduma zetu na kuongeza udahili wa wanafunzi, huku tukitumia fursa za kipekee za eneo hili kama utalii na biashara,” alisema Prof. Lwoga.

Alisema tawi hilo litatumika kutoa mafunzo katika fani mbalimbali ikiwemo masuala ya biashara, utalii na ujasiriamali, ili kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa nchi.


Naye mdau wa maendeleo kutoka Wilaya ya Hai, Joseph Mselee, alipongeza hatua hiyo akisema ni mkombozi kwa wananchi wa Kilimanjaro na maeneo jirani ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikosa huduma za elimu ya juu katika sekta ya biashara.

"Ujio wa chuo hiki utaleta manufaa makubwa kwa wananchi, wafanyabiashara wa mkoa wa Kilimanjaro watanufaika na elimu ya biashara, na hata shughuli za ujenzi wa chuo hicho zitaleta ajira na fursa za kiuchumi kwa wakazi wa eneo hili,” alisema Mselee.

Aliongeza kuwa mafunzo yatakayotolewa na chuo hicho yatakuwa msaada mkubwa kwa vijana na wajasiriamali waliopo katika mazingira ya kibiashara wilayani Hai na mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla.

Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) ni taasisi ya elimu ya juu iliyoanzishwa mwaka 1965 na kuthibitishwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE). Chuo hutoa mafunzo katika ngazi ya Cheti, Stashahada na Shahada katika fani mbalimbali za biashara na utawala.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.