BEST SIMBA; HAKUNA SABABU YA KUMUACHA RAIS SAMIA OKTOBA 29.

RAU-MOSHI.

Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Best Simba, amesema hakuna sababu yoyote kwa wananchi kuacha kumpigia kura mgombea urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Simba ambaye pia ni Mratibu wa Kampeni wa Wilaya ya Moshi Mjini, alitoa kauli hiyo Septemba 28, mwaka huu, katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za mgombea udiwani wa Kata ya Rau, Stallone Malinda, uliofanyika katika viwanja vya wazi vya Rau Madukani, na kuhudhuriwa na mamia ya wakazi wa eneo hilo.

“Serikali inayoongozwa na Rais Samia imeleta utulivu, umoja, na maendeleo makubwa kwa wananchi, hakuna sababu ya kumwacha mtu kama huyu kwenye uchaguzi ujao,” alisema Simba.

Aliongeza kuwa kazi iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ni ushahidi tosha wa dhamira ya CCM katika kuboresha maisha ya wananchi, hususan katika sekta za afya, elimu, miundombinu na huduma za kijamii.

Kwa mujibu wa Simba, wananchi wa Kata ya Rau na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla wanapaswa kuonesha shukrani kwa kazi hiyo kwa kumpigia kura mgombea urais wa CCM pamoja na wagombea wa ubunge na udiwani kupitia chama hicho.

“Kura tatu kwa CCM, urais, ubunge na udiwani, ndiyo jibu la kuthamini kazi iliyofanyika, tunawaomba wananchi wote, hata wale wa vyama vya upinzani, wajitokeze kumpigia Dk. Samia kwa sababu safari yao ya kushika dola bado ni ndefu sana,” alisema.

Katika mkutano huo, Simba aliwasihi wananchi kuendelea kudumisha amani na mshikamano katika kipindi chote cha kampeni na uchaguzi, huku akiwataka wagombea wa CCM kuwa mstari wa mbele kuwasikiliza na kuwahudumia wananchi wa maeneo yao.














Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.