RAU-MOSHI
Mgombea udiwani wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Rau, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Stallone Malinda, amesema Kata ya Rau inahitaji kiongozi mwenye msukumo na uwezo wa kupigania maendeleo ya kweli kwa wananchi, hususan katika maeneo ya miundombinu, afya na biashara ndogo.
Akizungumza Septemba 28, 2025, katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni zake uliofanyika kwenye viwanja vya wazi vya Rau Madukani, Malinda alisema moja ya vipaumbele vyake ni kupigania maboresho ya soko la Rau, ambalo alisema limekuwa na changamoto kubwa kwa miaka mingi.
“Soko la Rau halina miundombinu ya kisasa, kipindi cha mvua wafanyabiashara wanavujiwa, na wakati wa jua kali, hawana hata pa kujisitiri soko halina vyoo, wala huduma ya maji, haiwezekani wananchi watozwe ushuru kila siku lakini hawajawahi kuona maboresho,” alisema.
Alieleza kuwa endapo atapewa ridhaa ya kuwa diwani, atahakikisha suala la ujenzi wa soko jipya la kisasa linalokidhi mahitaji ya wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali linapewa kipaumbele katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.
Akizungumzia huduma za afya, Malinda alisema Zahanati ya Kata ya Rau inahitaji maboresho ya haraka, ikiwa ni pamoja na kuongezewa madaktari, wahudumu wa afya, na vifaa tiba ili wananchi wasilazimike kusafiri hadi KCMC au kata nyingine kutafuta matibabu.
Aidha, Malinda alieleza kuwa changamoto ya miundombinu ya barabara za ndani ni kubwa, akitaja baadhi ya barabara kama Kariwa Chini na Karikacha kuwa hazipitiki wakati wa mvua.
Alisema barabara za ndani zenye urefu wa zaidi ya kilomita 343.9 zinahitaji juhudi za makusudi kutoka kwa diwani atakayepigania bajeti ya ujenzi wake.
“Kata yetu inahitaji mtu wa kwenda kuziombea fedha hizi Halmashauri, mtu ambaye yuko tayari kusimama kwa ajili ya maslahi ya wananchi, si wa kupiga porojo,” alisisitiza Malinda.
Katika sekta ya ulinzi na usalama, Malinda aliahidi kusimamia maboresho ya kituo cha polisi cha kata hiyo ili kiweze kutoa huduma bora kwa wakazi wa Rau, na kuhakikisha mazingira bora ya kufanyia kazi kwa askari.
Kuhusu fursa za kiuchumi, Malinda aliahidi kuhakikisha kuwa vikundi vyote vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika kata hiyo vinapata mikopo ya asilimia 10 kutoka Halmashauri, kama ilivyoelekezwa kwenye mwongozo wa serikali.
“Ajenda hizi zote ninazozisemea leo zimeainishwa kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030, na ndizo msingi wa kuinua maendeleo ya wananchi wa Kata ya Rau, tukifanya kazi kwa pamoja, tunaweza,” alisema.














