MOSHI-KILIMANJARO.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Moshi imepokea Sh Bilioni 22.9 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara na mifereji ya maji ya mvua katika kata nane kati ya kata 21 za Manispaaya hiyo, kupitia Mradi wa TACTIC unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Fedha hizo zitatumika katika ujenzi wa jumla ya kilomita 13.2 za barabara za kiwango cha lami, ikiwemo barabara ya Ruwaichi hadi Njoro (km 6.9), barabara ya Pepsi (km 1.25), na barabara ya Shirimatunda hadi Magereza yenye urefu wa kilomita 5.1.
Pia, kutajengwa mifereji ya maji ya mvua katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mtaro kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika (MoCU), kupitia Key’s Hotel hadi Moshi Pazuri (km 2.0), na mtaro wa Kibong’oto (km 1.9), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupambana na changamoto za mafuriko wakati wa mvua.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba ya utekelezaji wa mradi huo iliyofanyika katika Kata ya Ng’ambo, Mratibu Msaidizi wa Mradi wa TACTIC kutoka Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Emmanuel Manyanga, alisema kuwa mradi huo unatekelezwa na Serikali Kuu kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia, na unalenga kuboresha huduma za miundombinu katika miji 45 nchini.
“Manispaa ya Moshi ni miongoni mwa Miji 15 ya kundi la pili inayonufaika na Awamu ya Pili ya mradi huu, mkandarasi aliyepatikana ni M/S Hari Singh and Sons Ltd kwa kushirikiana na Kampuni ya Peritus Exim Private Limited,” alisema Mhandisi Manyanga.
Aliongeza kuwa mradi wa TACTIC, wenye thamani ya dola za Marekani milioni 410, unalenga pia kuongeza uwezo wa taasisi katika usimamizi wa Miji na ukusanyaji wa mapato, sambamba na kuboresha huduma kwa wananchi.
Awali akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa barabara na mitaro ya maji ya mvua, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Mwajuma Nasombe, alisema Kata ya Ng’ambo ni miongoni mwa kata nane zitakazonufaika na utekelezaji wa mradi wa TACTIC, unaolenga kuboresha miundombinu ya barabara na mifereji ya maji ya mvua katika Manispaa hiyo.
Nasombe alieleza kuwa kupitia mradi huo, jumla ya kilomita 14 za barabara za lami na kilomita 4 za mifereji ya maji ya mvua zitajengwa, hatua inayotarajiwa kubadilisha sura ya mji wa Moshi na kuongeza hadhi ya maeneo ya pembezoni.
Aidha, alibainisha kuwa Kata ya Ng’ambo pia ni eneo linalojengwa hospitali kubwa ya wilaya yenye ghorofa, ambayo ni ya kisasa na ya kwanza ya aina hiyo katika mkoa wa Kilimanjaro, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, alisema kuwa mradi huo wenye thamani ya Shi bilioni 22 ni hatua muhimu ya kuondoa kero ya miundombinu duni kwa wakazi wa Manispaa ya Moshi, hususan walioko pembezoni mwa mji.
Babu aliwataka Wakandarasi waliokabidhiwa kazi hiyo kuhakikisha wanatekeleza mradi kwa viwango vya juu kama walivyoaminiwa na serikali, ili kufikia matarajio ya wananchi wanaosubiri kwa hamu kuona barabara bora na mifereji thabiti ya kupitisha maji ya mvua.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa mkoa alikemea vikali tabia ya baadhi ya wananchi wanaojihusisha na wizi wa vifaa vya ujenzi kutoka kwa wakandarasi, hali inayochelewesha utekelezaji wa miradi.
"Zipo tabia mbaya sana, wakandarasi wamekuwa wakilalamika kuwa vifaa kama mafuta na nondo vinapotea, hii siyo sawa, ni vyema tukalinda na kuthamini uwekezaji huu wa serikali kwa manufaa ya wote," alisisitiza RC Babu.
Mradi wa TACTIC unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya miundombinu ndani ya Manispaa ya Moshi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali ya awamu ya sita kuboresha maisha ya wananchi kupitia miradi mikubwa ya maendeleo.


















