MOSHI-KILIMANJARO.
WAKANDARASI wanaotekeleza miradi ya barabara mkoani Kilimanjaro wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaamini na kuwapatia kazi mbalimbali za ujenzi wa barabara, wakisema hali hiyo imeongeza ufanisi na uhakika wa malipo kwa wakati.
Shukrani hizo zilitolewa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Ujenzi ya M/S Hari Singh and Sons Ltd, Mhandisi Gurjit Dhani, mara baada ya kusaini mkataba na Wakala wa TACTIC kwa ajili ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 13.2 na mitaro ya maji ya mvua yenye urefu wa kilomita 3.9. Hafla ya utiaji saini ilifanyika katika Kata ya Ng’ambo, wilayani Moshi mkoani humo.
“Tunaishukuru sana Serikali ya Tanzania kwa kutuamini sisi wakandarasi wazawa na kutupatia kazi nyingi za maendeleo, tutaifanya kazi hii kwa weledi mkubwa ili wananchi wa Manispaa ya Moshi waweze kufaidika,” alisema Mhandisi Dhani.
Alisema mradi huo unatarajiwa kuanza rasmi tOktoba mosi mwaka huu na utakamilika ndani ya miezi 15 kama ilivyoainishwa katika mkataba.
“Tunaahidi kutekeleza mradi huu kwa kasi na ubora wa hali ya juu ili kuonesha kuwa wakandarasi wazawa wanaweza kufanya kazi kubwa kwa ufanisi,” aliongeza.
Mhandisi Dhani alisema changamoto zilizokuwepo awali ni pamoja na ukosefu wa kazi na ucheleweshaji wa malipo, hali iliyosababisha baadhi ya miradi kuchelewa kukamilika, hata hivyo, alisema tangu kuingia madarakani kwa Rais Samia, mambo yamebadilika kwa kiwango kikubwa.
“Kwa sasa, serikali inalipa kwa wakati, na kazi zipo, hli ni jambo kubwa kwetu wakandarasi,” alisema.
Aidha, aliomba Serikali kuendelea kuwaamini wakandarasi wazawa na wadogo kwa kuwapatia miradi zaidi, jambo ambalo litawajengea uwezo wa kifedha na kiuzoefu, na hatimaye kuchochea ukuaji wa sekta ya ujenzi nchini.
Pia, aliwataka wakandarasi wenzake kuwa wazalendo kwa kufanya kazi kwa uadilifu na kuzingatia viwango vya ubora, ili kusaidia serikali kutimiza malengo yake ya kuboresha miundombinu ya barabara nchini.
Mratibu Msaidizi wa Mradi wa TACTIC kutoka Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Emmanuel Manyanga, alisema kuwa mradi huo unatekelezwa na Serikali Kuu kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia, na unalenga kuboresha huduma za miundombinu katika miji 45 nchini.
Alisema kwa Manispaa ya Moshi, mradi unakwenda kutekelezwa kwa kiasi cha Sh bilioni 22.9 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya barabara na mifereji ya maji ya mvua katika kata nane, kati ya 21 za Manispaa hiyo, kupitia Mradi wa TACTIC unaofadhiliwa na Benki ya Dunia.
"Barabara zitakazojengwa kwa kiwango cha lami ni pamoja na Ruwaichi–Njoro (km 6.9), Pepsi (km 1.25), na Shirimatunda–Magereza (km 5.1). Vilevile, mitaro ya maji ya mvua itajengwa katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika (MoCU) kupitia Key’s Hotel hadi Moshi Pazuri (km 2.0), na mtaro wa Kibong’oto (km 1.9).
"Mradi huu, unalenga kukabiliana na changamoto za mafuriko katika Manispaa hiyo, hasa wakati wa mvua kubwa,"alisema.
Mkazi wa Msaranga, Kata ya Ng’ambo, Romel Mosha, ameipongeza serikali kwa kuleta mradi huo katika eneo lao, akisema kuwa walikuwa wakikumbwa na mafuriko ya mara kwa mara kila mvua zinaponyesha.
“Mradi huu utaleta mabadiliko makubwa, kukamilika kwa barabara kutatoa fursa zaidi za kiuchumi na biashara kwa wakazi wa eneo hili,” alisema.







