WAKAZI WA KATA YA MIEMBENI, WAELEZA KILIO CHAO KWA MGOMBEA UDIWANI

MJI MWEMA- MIEMBENI.

Wakazi wa Kata ya Miembeni, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wamemuomba mgombea udiwani wa kata hiyo, Haruna Ally Mushi, kushughulikia changamoto sugu zinazowakabili pindi atakapochaguliwa, ikiwemo ukosefu wa zahanati, kituo cha polisi, soko la mazao, uwanja wa michezo, pamoja na ubovu wa miundombinu ya barabara.

Wakizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika eneo la Mji Mwema-Makutini, wananchi walisema wamekuwa wakiishi na changamoto hizo kwa muda mrefu bila ya kupatiwa suluhisho, hali inayowaathiri kijamii na kiuchumi.

Mkazi wa Mji Mwema, Yesaya Masaoe, alisema kutokana na kukosekana kwa zahanati katika kata hiyo, wagonjwa hulazimika kupelekwa kwenye kata za jirani kama Majengo, Pasua na Mji Mpya, jambo linalowasababishia usumbufu mkubwa, hasa wakati wa dharura.

"Kata yetu haina kituo cha polisi, zahanati, barabara ni mbovu, na nyumba nyingi hazina hati miliki, tunamuomba diwani atakayechaguliwa kushughulikia haya kwa haraka," alisema Masaoe.

Naye mkazi mwingine, Agnes Kambi, alieleza kuwa ukatili wa kijinsia na kutowajibika kwa wazazi katika malezi ya watoto ni changamoto nyingine kubwa inayolikabili eneo hilo.

Alisema shule nyingi zinashindwa kutoa chakula cha mchana kwa wanafunzi kutokana na wazazi kushindwa kulipia gharama hizo.

"Wazazi wapo tayari kuchangia harusi kwa shilingi 50,000 hadi 100,000 lakini wanashindwa kuchangia shilingi 60,000 kwa mwaka kwa ajili ya chakula cha mtoto wao shuleni, diwani ajaye aweke msukumo katika elimu ya malezi na uwajibikaji wa wazazi," alisema Kambi.

Kwa upande wake, Ramadhani Mussa Alli, mkazi wa Miembeni, alisema kata hiyo inakabiliwa pia na ukosefu wa soko, uwanja wa michezo, pamoja na kutokuwepo kwa uzio kwenye shule ya msingi Miembeni, JK Nyerere Sekondari na shule mpya ya Mji Mpya.

Akihutubia mkutano huo wa hadhara, mgombea udiwani wa kata hiyo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Haruna Ally Mushi, aliwahakikishia wakazi wa Miembeni kuwa endapo atachaguliwa, atatumia nafasi yake ndani ya baraza la madiwani kushinikiza utekelezaji wa miradi muhimu ya maendeleo katika kata hiyo.

"Changamoto hizi nyingi ninazifahamu, na nyingine mmekuwa mkinieleza, naombeni kura zenu ili niende halmashauri kulishauri baraza kwa bidii na kuhakikisha tunapata zahanati, kituo cha polisi, ofisi ya kata, na huduma nyingine muhimu," alisema Mushi.

Aidha, Mushi aliahidi kuwa atahakikisha asilimia 10 ya mapato ya halmashauri inayotakiwa kutolewa kama mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, inawafikia walengwa kwa wakati bila urasimu.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.