MGOMBEA UDIWANI PASUA ATANGAZA VIPAUMBELE VITATU VYA MAENDELEO, KUANZA NA ZAHANATI


PASUA-MOSHI.

Mgombea Udiwani wa Kata ya Pasua katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Barreh Farrah, ametangaza vipaumbele vyake vitatu kwa wapiga kura wa kata hiyo, akisisitiza dhamira yake ya kuhakikisha Pasua inapata zahanati ya kisasa endapo atachaguliwa kuwa diwani.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo la Kwa Bwerere-Matindigani, Farrah alisema kata ya Pasua imekosa zahanati kwa muda mrefu hali inayowalazimu wananchi kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya.

"Ndani ya siku 60 baada ya kuchaguliwa, nitaanza haraka kushirikiana na madiwani wenzangu kuhakikisha tunaanzisha mchakato wa kuipatia Pasua zahanati, hili ni hitaji la msingi kwa wananchi wetu," alisema Farrah.

Katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa pia na mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kupitia CCM, Ibrahim Shayo maarufu kama ‘Ibra Line’, Farrah alieleza kuwa atasimamia matumizi ya rasilimali zilizopo ndani ya kata kwa manufaa ya vijana, ikiwa ni sehemu ya ajenda yake ya ajira.

Alisema moja ya nguvu kubwa aliyonayo ni mahusiano mazuri na wadau mbalimbali, jambo litakalomsaidia katika kuvutia maendeleo na uwekezaji katika kata hiyo.

"Nina maono makubw5a kwa Pasua, kwa kushirikiana nanyi wananchi, tutatumia rasilimali zilizopo ndani ya kata kuwawezesha vijana kupata ajira na kuboresha maisha yao," aliongeza.

Aidha, Farrah aliahidi kupigania upatikanaji wa bima ya afya kwa wazee, ili waweze kupata matibabu bila usumbufu katika hospitali mbalimbali.

"Ndugu zangu wana Pasua, naomba ridhaa yenu niwe mwakilishi wenu kwenye Baraza la Madiwani, nitahakikisha wazee wetu wanapata bima ya afya na huduma bora za matibabu," aliahidi.

Akihitimisha hotuba yake aliyotumia dakika nane, aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, mwaka huu, kuwachagua wagombea wa CCM katika ngazi zote kwa ajili ya kulinda na kuendeleza misingi ya maendeleo ya taifa.













Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.