MIEMBENI-MOSHI.
Mgombea udiwani wa Kata ya Miembeni kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Haruna Mushi, amesema kuwa endapo atachaguliwa, atahakikisha anatekeleza mikakati ya maendeleo kwa kasi inayolingana na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni uliofanyika katika eneo la Dampo, Mtaa wa Arabika, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Mushi alisema Dira hiyo mpya itakuwa mkombozi kwa mwananchi mmoja mmoja katika kukuza na kuinua kipato chao cha kila siku.
"Ni wakati wa kuijenga Kata ya Miembeni Mpya, nitahakikisha kila mwananchi anapata nafasi ya kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kata hii, kwa kuzingatia Dira ya Taifa ambayo inalenga kumwinua Mtanzania mmoja mmoja," alisema Mushi mbele ya umati wa wakazi wa Miembeni.
Alisema Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 imeweka mkazo katika kuboresha maisha ya wananchi kwa kuhakikisha kunakuwa na uchumi imara, uwazi katika uongozi, na ushiriki wa kila mmoja katika maendeleo, mimi nimejipanga kuisukuma Miembeni kwenda sambamba na dira hiyo.
Akitaja vipaumbele vyake, Mushi alisema moja ya maeneo atakayoyapa kipaumbele ni uboreshaji wa miundombinu ya barabara ili kurahisisha usafiri na shughuli za kiuchumi kwa wananchi.
Aidha mgombea udiwani huyo, aliahidi kwenda kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa Kata ya Miembeni ikiwemo miundombinu mibovu ya barabara, ajira kwa vijana, huduma bora za afya na elimu, pamoja na kuweka mazingira rafiki kwa biashara ndogondogo.
Kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa makundi maalum, Mushi aliahidi kuwa atasimamia kwa ukamilifu upatikanaji na usambazaji wa mikopo hiyo kwa haki, ili kuhakikisha vijana, wanawake na watu wenye ulemavu wanapata fursa sawa za kiuchumi.
"Mikopo hii haitakuwa kwa wachache wala kwa upendeleo, tunataka kila mmoja aweze kunufaika na mikopo hiyo kwa usawa na uwazi," alisisitiza.
Aidha, aliwahamasisha wananchi wa Kata ya Miembeni kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, mwaka huu, kushiriki katika uchaguzi kwa kuwachagua wagombea wa CCM kuanzia ngazi ya urais, ubunge hadi udiwani, kwa ajili ya kuleta maendeleo endelevu.















