TRA KILIMANJARO YAWASHUKURU WAFANYABIASHARA KWA KUVUKA LENGO LA MAKUSANYO

MOSHI-KILIMANJARO.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro imewashukuru wafanyabiashara na walipa kodi wote mkoani humo kwa kushiriki kikamilifu katika ulipaji wa kodi, hali iliyoiwezesha mamlaka hiyo kufanikisha na kuvuka lengo la makusanyo kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Akizungumza leo Septemba 23,2025 katika hafla fupi ya uzinduzi wa Dawati Maalum la Uwezeshaji Biashara mkoani hapa, Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro, James Jilala, alisema kuwa katika mwaka huo wa fedha, lengo la makusanyo lilikuwa Shilingi bilioni 301.64, huku makusanyo halisi yakiwa Shilingi bilioni 330.81, sawa na asilimia 110 ya lengo.

“Tunawashukuru sana walipa kodi kwa uaminifu na uzalendo wao, mafanikio haya ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya TRA na wafanyabiashara, pamoja na juhudi kubwa za watumishi wetu,” alisema Jilala.

Kwa upande mwingine, Jilala alisema kuwa katika kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara nchini, serikali kupitia TRA imezindua Dawati Maalum la Uwezeshaji Biashara ambalo litatoa huduma karibu zaidi kwa wafanyabiashara na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ya kikodi kwa ufanisi.

“Uzinduzi huu ni sehemu ya juhudi za serikali katika kuhakikisha mazingira bora ya kufanya biashara, kwa kutoa elimu, ushauri, na msaada wa karibu kwa walipa kodi,” aliongeza.

Akizindua rasmi dawati hilo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, aliwahimiza wananchi kuendelea kujisajili kikamilifu, kuwasilisha ritani kwa wakati, kutoa taarifa sahihi na kulipa kodi kwa mujibu wa sheria.

“Niwapongeze Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro na watumishi wote kwa kufanya kazi kwa weledi, uwajibikaji na uadilifu, hali hii imechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha makusanyo na kuvuka lengo mlilopangiwa,” alisema RC Babu.

Akizungumzia umuhimu wa dawati hilo, Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa litasaidia kuondoa vikwazo vya kibiashara, kutoa elimu ya kodi, na kusaidia sekta binafsi kuchangia kikamilifu katika kukuza uchumi wa ndan

“Kupitia dawati hili, wafanyabiashara watapata taarifa sahihi kwa wakati, kuelewa haki na wajibu wao wa kikodi, pamoja na kusaidiwa kutatua changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika shughuli zao za kila siku,” alifafanua.

Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Yusuph Nzowa, aliipongeza TRA kwa kuanzisha dawati hilo, akisema hatua hiyo inalenga kujenga uhusiano mzuri na wa karibu zaidi kati ya TRA na wafanyabiashara.

“Hapo awali kulikuwepo na dhana potofu kuwa wafanyabiashara na TRA ni mahasimu, lakini kwa sasa hali ni tofauti, Dawati hili litasaidia kuwaunganisha na kuimarisha uhusiano huo,” alisema Nzowa.

Aidha, alihimiza wafanyabiashara kulitumia kikamilifu dawati hilo kama daraja la mawasiliano, ushauri na msaada wa kikodi, ili kufanikisha malengo ya biashara na maendeleo ya uchumi kwa ujumla.

















Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.