NJORO-MOSHI
Meya wa zamani wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Zuberi Abdallah Kidumo, ameahidi kuboresha Uwanja wa Netball wa Reli uliopo Kata ya Njoro, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhamasisha ushiriki wa wasichana na wanawake katika michezo, hususan mchezo wa netball.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja huo, Kidumo alisema hatua hiyo inalenga kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza michezo nchini, na kuhakikisha hakuna michezo inayosahaulika huku nguvu nyingi zikiendelea kuelekezwa kwenye soka.
“Michezo mingi imekuwa ikisahaulika huku nguvu nyingi zikiwekezwa kwenye soka, kupitia maboresho haya, tunalenga kuwahamasisha wanawake na wasichana kushiriki kwa wingi katika mchezo wa netball,” alisema Kidumo.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi (CCM), akiwemo mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kupitia CCM, Ibrahim Shayo.
Kidumo alibainisha kuwa baada ya kumalizika kwa mashindano ya mpira wa miguu yanayoendelea hivi sasa chini ya jina la Zuberi Cup, juhudi kubwa zitaelekezwa katika kuboresha uwanja wa netball, ikiwa ni maandalizi ya kuanzisha mashindano ya kila mwaka ya netball.
“Baada ya Zuberi Cup, nguvu kubwa itaelekezwa kwenye uwanja wa netball ili kuandaa mazingira bora ya kufanikisha michuano ya kila mwaka,” alieleza.
Aidha, Mhandisi Kidumo aliahidi kuhakikisha taa zinawekwa katika viwanja vyote vya netball na mpira wa miguu ili kuwezesha mazoezi na mechi kufanyika hata wakati wa usiku.
![]() |
![]() |










