KIUSA-MOSHI.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ibrahim Shayo, ameendelea kuinadi Ilani ya uchaguzi
ya CCM kwa wananchi wa Manispaa ya Moshi kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
ya CCM kwa wananchi wa Manispaa ya Moshi kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Akizungumza na wakazi wa Kata ya Kiusa katika mkutano wa kampeni uliofanyika Septemba 22, 2025 katika eneo la Maduka Mpangano (Seven Eleven), Shayo aliwataka wananchi kuichagua CCM kwa kuwa ndicho chama pekee kinachosikiliza na kutatua changamoto za wananchi.
"CCM imeendelea kuwa sikio la wananchi. Ilani yetu inajieleza wazi — tumejipanga kuboresha maisha ya kila Mtanzania kupitia sekta muhimu kama afya, uchumi na miundombinu," alisema Shayo.
Alibainisha kuwa katika Manispaa ya Moshi, Ilani ya CCM itaendelea kuboresha huduma za afya kwa kuhakikisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya katika Kata ya Ng’ambo unakamilika na kuanza kutoa huduma bora kwa wananchi.
Vilevile, aliahidi kuimarisha uchumi wa wananchi kwa kuongeza fursa za kipato, kuimarisha ustawi wa jamii na kuboresha hali ya maisha kwa ujumla.
Akizungumzia miundombinu, Shayo alisema CCM imepanga kuboresha barabara zote za ndani ya Manispaa ya Moshi kwa kiwango cha lami na changarawe, hatua itakayorahisisha usafiri na kuinua maendeleo ya mji.
Aliwataka wananchi wa Moshi Mjini na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla kumpigia kura Dk. Samia Suluhu Hassan kwa nafasi ya urais, pamoja na wagombea wa CCM katika nafasi za ubunge na udiwani.
Hadi sasa, mgombea huyo ameshafanya kampeni katika kata mbalimbali zikiwemo Korongoni, Mfumuni, Kaloleni, Ng’ambo, Njoro, Kiboriloni, Mji Mpya, Pasua na Kiusa.




















