KIUSA, MOSHI
Mgombea udiwani Kata ya Kiusa, Khalid Shekoloa, ameeleza vipaumbele vitano vya maendeleo kwa kata hiyo, huku akimuomba mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ibrahim Shayo, kuhakikisha anapigania kuboreshwa kwa makazi ya askari polisi endapo atachaguliwa kuwa Mbunge.
Akizungumza Septemba 22, 2025, kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika eneo la Maduka Mpangano, Kata ya Kiusa, Manispaa ya Moshi, Shekoloa alisema makazi ya askari polisi eneo la Kiusa Laine yamekuwa changamoto kubwa kwa muda mrefu, hali inayodhoofisha hali ya maisha na morali ya askari hao.
"Nakuomba Mbunge mtarajiwa, ukachukue kilio hiki cha muda mrefu cha askari wetu. Nyumba zao hazina hadhi ya kuishi, tunahitaji kuona bunge likitenga fedha kwa ajili ya makazi bora ya askari polisi," alisema Shekoloa.
Aidha, Shekoloa aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuleta fedha za maendeleo katika sekta ya elimu, hasa katika ukarabati wa shule kongwe kama shule ya msingi Mwenge, hata hivyo, alieleza kuwa bado shule nyingine kama Jamhuri na Muungano zinakabiliwa na changamoto mbalimbali.
"Shule ya Msingi Jamhuri haina ukuta wala uzio, jambo linalohatarisha usalama wa wanafunzi, shule ya Muungano nayo inahitaji ukarabati mkubwa, tunaomba Mbunge ukalisimamie hili," aliongeza.
Akigusia hali ya miundombinu, Shekoloa alisema barabara za ndani, hasa eneo la Kiusa Laine, zimekuwa kero ya muda mrefu, alitaja barabara ya Nyasa kwa Mzee Minja na barabara ya Lusaka (Mkulima) inayotoka Marangu Shaine kuwa miongoni mwa barabara zinazohitaji ukarabati wa haraka.
Kwa upande wa huduma za maji taka, alisema mfumo uliopo kati ya Police Line na Kiusa Laine ni mdogo na umekuwa ukileta usumbufu mkubwa kwa wakazi wa maeneo hayo.
Diwani huyo pia aligusia changamoto ya utoaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Alisema licha ya wananchi kujitokeza na kujaza fomu kwa usahihi, fedha hizo zimekuwa zikicheleweshwa kwa sababu ya urasimu mkubwa unaodaiwa kufanywa na baadhi ya watendaji.
"Wananchi wanalalamika kwamba kuna maafisa maendeleo ya jamii wanaotaka kupewa asilimia 10 ya fedha hizo kabla hazijatolewa, urasimu huu ni lazima uondolewe, nkichaguliwa Oktoba 29, nitaenda kuufuatilia kwa karibu hadi ukome," alisema kwa msisitizo.
Akihitimisha, Shekoloa aliwaomba wananchi wa Kiusa kumpigia kura Mbunge Ibrahim Shayo, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na madiwani wote wa CCM, akisisitiza kuwa kura zote 5,318 za wapiga kura waliojiandikisha Kata ya Kiusa zielekezwe kwa CCM ili kufanikisha maendeleo zaidi.
















