IBRAHIM SHAYO; ASILIMIA 80 YA MAPATO YANGU HUYATUMIA KUSAIDIA JAMII

MJI MPYA-MOSHI.

Mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ibrahim Shayo, amesema kuwa kwa kipindi kirefu amekuwa akitumia asilimia 80 ya mapato yake binafsi kusaidia jamii, akisisitiza kuwa hiyo ni dhamira yake ya dhati ya kuwatumikia wananchi hata kabla hajawa kiongozi wa kisiasa.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo katika eneo la Mchomba, Kata ya Mji Mpya, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Shayo alibainisha kuwa uwezo wake wa kusaidia haukutokana na madaraka, bali ni moyo wake wa kujitoa kwa jamii.

"Asilimia 80 ya mapato yangu nayatumia kusaidia jamii, kama nimeweza kufanya hivi kabla sijawa mbunge, leo nakuja kuwaomba kura zenu, mnichague niwe mwakilishi wenu bungeni, nami nitafanya mara mbili ya kile nilichokuwa nikitoa hapo awali," alisema Shayo mbele ya umati wa wakazi wa Mji Mpya.

Shayo abaye pia ni mzaliwa wa kata hiyo, aliahidi kushughulikia changamoto ya miundombinu ya barabara katika maeneo ya pembezoni mwa mji, akisema kuna maeneo mengi ambayo yamesahaulika na yanahitaji uboreshaji wa haraka ili kuwezesha huduma bora kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, mgombea huyo alitumia fursa hiyo kumuombea kura Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, diwani wa kata hiyo ambaye pia ni Kaka yake Abuu Mohamed Shayo, akimtaja kama kiongozi mwenye maono makubwa aliyefanikisha maendeleo makubwa katika kata hiyo.

"Rais Samia ametuletea fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya inayojengwa kata ya Ng’ambo, pia ametuwezesha kukarabati shule kongwe, ni wakati wetu sasa kumrudishia heshima kwa kumpa kura nyingi," alisema mgombea Ubunge Shayo.

Ibra Shayo alihitimisha kwa kuwataka wananchi wa Moshi Mjini kumpigia kura yeye, Rais Samia pamoja na mgombea udiwani wa kata hiyo Abuu Shayo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, ili kwa pamoja washirikiane kuleta maendeleo makubwa zaidi kwa mji wa Moshi.










Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.