CHAMARUKI WAJITOLEA KUKARABATI JENGO LA POLISI WILAYA YA MOSHI

MOSHI-KILIMANJARO.

Chama cha Wajenzi na Wapiga Rangi Mkoa wa Kilimanjaro (CHAMARUKI) kimeonyesha uzalendo kwa vitendo baada ya kujitolea kukarabati jengo la kituo cha polisi Wilaya ya Moshi, ikiwa ni sehemu ya mchango wao kwa jamii na taasisi za umma.

Akizungumza jana katika hafla fupi ya utambulisho wa bidhaa za ujenzi zinazozalishwa hapa nchini na Kampuni ya FATU 45 CO. LTD ya Jijini Arusha, Katibu Mtendaji wa CHAMARUKI mkoa wa Kilimanjaro, Casmiry John Toto, alisema uamuzi huo umechukuliwa kufuatia ombi la Mkuu wa Kituo cha Polisi Moshi (OCD), ambaye aliomba msaada wa mafundi kutoka chama hicho kwa ajili ya ukarabati wa jengo hilo.

“Mkuu wa kituo aliniomba binafsi tuweze kuwasaidia kukarabati jengo la polisi, kama mtendaji mkuu wa CHAMARUKI, tuliona ni wajibu wetu kulifanyia kazi ombi hilo kwa sababu jengo lile ni mali ya umma na linahudumia wananchi wote,” alisema Toto.

Aliongeza kuwa kupitia ushirikiano na kampuni ya FATU 45 CO. LTD, kazi hiyo ya ukarabati itatekelezwa kwa pamoja ambapo CHAMARUKI watatoa nguvu kazi, huku kampuni hiyo ikiahidi kuchangia fedha na vifaa vitakavyohitajika.

“Niliwasiliana na Mkurugenzi wa FATU 45 CO. LTD, tukamweleza nia yetu ya kuchangia kwa hali na mali, kwa moyo wa uzalendo, alikubali kuwa sehemu ya mradi huu wa kijamii,” alieleza Katibu huyo.

Aidha, Katibu huyo aligusia changamoto zinazokikumba chama hicho, hususan ukosefu wa nafasi katika zabuni mbalimbali za serikali, licha ya kuwa chama chenye usajili rasmi.

“Tunaiomba serikali, pindi kunapotangazwa tenda zinazohitaji mafundi ujenzi au wapiga rangi, basi na sisi CHAMARUKI tuweze kupewa nafasi, tuna uwezo na wataalamu waliobobea,” alisema Toto.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa FATU 45 CO. LTD, Omari Mohamed Ndwatta, aliwasihi mafundi wajenzi na wapiga rangi kutumia bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi kama njia ya kumuunga mkono Mtanzania mwenzetu na kukuza uchumi wa ndani.

“Bidhaa zetu ni bora na zinapatikana kwa bei rafiki, nawaomba muwe mabalozi wa bidhaa zetu na muendelee kufanya kazi kwa ubora na uaminifu mkubwa,” alisema Ndwatta.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, Afisa Tawala wa Wilaya ya Moshi, Theresia Mmbaga, aliwataka wanachama wa CHAMARUKI kujenga uaminifu katika kazi wanazofanya ili kuaminika na kupata kazi zaidi.

“Ni muhimu kusajiliwa kwenye mfumo wa serikali wa NEST ili kushiriki katika tenda mbalimbali zinazotangazwa,” alishauri.

Aidha, aliwapongeza viongozi wa CHAMARUKI kwa moyo wao wa kujitolea katika ukarabati wa jengo la polisi na kusema kuwa hatua hiyo inapaswa kuigwa na taasisi nyingine nchini.








Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.