KIDUMO AWATAKA WANANCHI WA NJORO KUMCHAGUA SAMIA, IBRAHIMU SHAYO NA WADIWANI WA CCM

KILIMANJARO.

Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, mgombea udiwani kata ya Njoro kupitia tiketi ya CCM, amewahimiza wananchi wa kata hiyo kumchagua mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, pamoja na mgombea ubunge wa jimbo la Moshi Mjini, Ibrahim Shayo na wadiwani wote wa chama hicho, ili kuendeleza maendeleo ya kata na jimbo kwa ujumla.

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 20, 2025, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa netball reli Njoro, ambapo Kidumo alisisitiza imani yake kubwa katika viongozi wa CCM kuwa wataweza kuleta mabadiliko chanya.

"Ushirikiano wenu ni nguzo ya mafanikio yetu, nina imani kubwa kuwa tutampa mgombea wetu wa ubunge, Ibrahim Shayo, kura nyingi, ili twende kwa pamoja kuleta maendeleo katika jimbo la Moshi Mjini na kata ya Njoro," alisema Kidumo huku akiwahimiza wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi.

Mhandisi Kidumo pia alitaja mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, akisema kata ya Njoro imefaidika moja kwa moja kupitia fedha za maendeleo zilizotolewa na serikali.

Akizungumzia uwanja wa netball reli Njoro, Kidumo aliahidi ujenzi wa uwanga na upandaji wa nyasi za kisasa ili kuifanya eneo hilo kuwa sehemu bora kwa ajili ya michezo na mazoezi, hasa kwa wanawake waliokuwa wakitumia uwanja huo jioni kwa shughuli za mwili.

"Tunataka kuona akina mama wakiendelea kutumia uwanja huu kwa shughuli za mazoezi, hivyo tutahakikisha uwanja huu unapewa mwanga wa kutosha ili kurahisisha mazoezi baada ya jioni," alisema Kidumo, huku akiongeza kuwa tayari amemuomba mgombea ubunge Shayo kuweka taa zitakazorahisisha shughuli za jioni uwanjani hapo.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, alitangaza mpango wake wa kuwasaidia vijana wanaojihusisha na biashara ya bidabida na bajaji kwa kuwapatia vyombo vya usafiri kupitia mikopo nafuu endapo atachaguliwa.

Mpango huo unalenga kuondoa changamoto za mikataba ya ukandamizaji kwa madereva, kwa kuwatafutia wafadhili watakaowezesha mikopo hiyo kwa masharti nafuu, ambapo madereva watakuwa na jukumu la kulipa kidogo kidogo kwa urahisi.

Ibrahim Shayo aliwahimiza wananchi kuendelea kumuunga mkono ili waweze kutekeleza ajenda za maendeleo zinazolenga kuleta usawa na ustawi wa kila mtu jimboni Moshi Mjini.

















Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.