MOSHI-KILIMANJARO.
Mgombea ubunge jimbo la Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, amewahakikishia wakazi wa mji huo kwamba atajitahidi kushughulikia changamoto ya miundombinu ya barabara hasa zile za pembezoni ambazo zimekuwa kikwazo kwa maendeleo ya mji.
Shayo alitoa ahadi hiyo leo, Septemba 20, 2025, wakati wa mkutano wake wa kampeni uliofanyika viwanja vya netball reli, kata ya Njoro, Moshi Mjini.
Akizungumza na wakazi wa kata ya Njoro, mgombea huyo alisema kuwa mojawapo ya mambo anayoyapigania ni kuleta maboresho ya barabara katika maeneo yaliyoathirika, na kuahidi kupeleka hoja bungeni ili kuomba serikali kuongeza fedha kwa ajili ya maendeleo ya miundombinu ya barabara katika Moshi.
“Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan, amefanya mambo mengi mazuri katika mji wetu wa Moshi, amesaidia halmashauri ya Manispaa yetu ya Moshi, kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali yetu ya wilaya inayojengwa kata ya Ng’ambo, "alisema
Pia alisema Rais Samia, alitoa fedha za ukarabati wa shule zetu za sekondari, kama vile Mawenzi Sekondari ambayo sasa imebadilika na hatimaye inakuwa kama makazi ya mtu binafsi,” alisema Shayo.
Aidha, alitoa wito kwa wana Moshi kumpa kura nyingi Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ili awe na nguvu ya kuendelea kutetea na kuwaletea maendeleo wananchi wa Moshi katika kipindi chake kijacho.
![]() |









