NJORO-MOSHI.
Taasisi isiyo ya kiserikali ya "KIJANA KWANZA" imetoa Sh milioni 195 kusaidia ujenzi na ukarabati wa Zahanati ya Njoro pamoja na ununuzi wa vifaa tiba, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Kata ya Njoro, Manispaa ya Moshi.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Uwanja wa Reli, Kata ya Njoro, Mstahiki Meya mstaafu wa Manispaa ya Moshi ambaye pia ni mgombea udiwani wa kata hiyo, Mhandisi Zuberi Abdallah Kidumo, aliishukuru taasisi hiyo kwa mchango mkubwa walioutoa katika kuboresha zahanati hiyo.
“Ninaishukuru sana taasisi ya "KIJANA KWANZA" kwa namna walivyonishika mkono, walitupatia zaidi ya Sh milioni 100 zilizotumika kukarabati zahanati yetu ya Njoro, iliyokuwa imechakaa sana,” alisema Kidumo.
Mhandisi Kidumo alieleza kuwa kupitia msaada huo, tayari jengo jipya la wodi ya mama na mtoto limekamilika, likiwa ni la kisasa kabisa, na kuongeza kuwa lengo ni kuifanya Zahanati ya Njoro kuwa kinara wa utoaji wa huduma bora za afya kwa mama na mtoto katika Manispaa ya Moshi.
"Zahanati hii sasa imepata hadhi mpya. Nataka niwaambie ukweli wananchi wa Njoro, nilipopokea fedha hizi sikuwahi kuwaambia kiasi halisi, lakini taasisi ya KIJANA KWANZA ilinipatia zaidi ya milioni 100, na kwa uaminifu wangu, kila senti imeelekezwa kwenye ukarabati,” alisema.
Mhandisi Kidumo, alisema baada ya kukamilika kwa ukarabati wa majengo, aliwasiliana tena na uongozi wa taasisi hiyo ya KIJANA KWANZA, kuwaomba msaada wa vifaa tiba, ambapo taasisi hiyo ilikubali kutoa Sh milioni 70 kwa ajili ya vifaa hivyo.
"Nilienda mwenyewe China kuchagua vifaa bora vinavyohitajika kwenye zahanati hii, tayari taasisi imelipia vifaa hivyo, na jana nilienda bandarini Dar es Salaam kulipia kodi zote kwa gharama yangu binafsi,” alisema.
Mhasibu wa "KIJANA KWANZA" Sadath Sudi Ndibalemwa, alithibitisha kuwa taasisi hiyo imetoa zaidi ya Sh milioni 195, ambapo Sh milioni 125 zilitumika katika ujenzi na ukarabati wa zahanati, na milioni 70 kwa ununuzi wa vifaa tiba.
“Tulisema hatuwezi kujenga jengo tu bila vifaa, tayari tumenunua vifaa tiba vyenye thamani ya milioni 70, na mwishoni mwa mwezi Septemba tutavikabidhi rasmi sambamba na uzinduzi wa jengo,” alisema Ndibalemwa.
Wananchi wa Kata ya Njoro wamepongeza mchango huo na kuonyesha matumaini kuwa huduma za afya zitaboreshwa zaidi kupitia ushirikiano kati ya viongozi wa eneo hilo na taasisi za kijamii kama Kijana Kwanza.











