IBRAHIM SHAYO; KUKIFUFUA KIWANDA CHA MAGUNIA MOSHI

PASUA-MOSHI.

Mgombea wa ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ibrahim Shayo, ameahidi kushirikiana na serikali kuhakikisha kiwanda cha magunia cha Moshi (Tanzania Bag Corporation) kinafufuliwa ili kiweze kusaidia kupunguza tatizo la ajira kwa wananchi wa jimbo hilo.

Shayo aliyasema hayo septemba 19,2025 wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika eneo la Matindigani-Pasua, mkutano ulioenda sambamba na kumnadi mgombe udiwani kata ya Pasua Barreh Farrah.

Alisema iwapo atapewa ridhaa ya kuwa Mbunge baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu, atapaza sauti ya wananchi bungeni kwa lengo la kufufua viwanda vilivyokufa.

“Kiwanda hiki kilianzishwa rasmi Machi 31, 1970 na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kiwqnda hiki kiliwahi kutoa ajira kwa mamia ya wananchi kabla ya kufungwa mwaka 1999 na kubinafsishwa, lakini leo hii kimebaki kuwa gofu,” alisema Shayo.

Mbali na kiwanda cha magunia, mgombea huyo aliahidi kufuatilia sababu za kufa kwa viwanda vingine muhimu vilivyokuwa vikiendesha uchumi wa mji wa Moshi, ikiwemo Kiwanda cha Ngozi cha Moshi, kiwanda cha Kibo Match pamoja na kiwqnda cha Kibo Paper.

"Viwanda hivi vilikuwa tegemeo kubwa kwa wakazi wa Moshi, nitahakikisha ninapata majibu ya sababu za kufa kwa viwanda hivi, na nitashirikiana na mamlaka husika kuvifufua ili kutoa ajira na kuchochea maendeleo ya mji wetu,” alieleza.







Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.