MOSHI-KILIMANJARO
Mgombea wa ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, ameahidi kushirikiana na Baraza la Madiwani la Manispaa ya Moshi kuhakikisha unapatikana mradi wa magari zaidi ya kuzoa taka, endapo atachaguliwa kuwa mbunge.
Shayo alitoa ahadi hiyo leo, Septemba 18, 2025, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Sekondari Muslim, iliyopo Kata ya Kaloleni.
Akihutubia wakazi wa kata hiyo, Shayo alisema licha ya Moshi kujulikana kwa usafi wake, kwa sasa mji huo unakabiliwa na changamoto ya mrundikano wa taka zinazozalishwa majumbani na viwandani kutokana na uhaba wa magari ya kuzoa taka.
“Mji wetu wa Moshi kwa sasa unakabiliwa na changamoto ya magari ya kuzoa taka. Mkinichagua kuwa mbunge wenu, nitashirikiana na madiwani kuongeza magari ya kuzoa taka ili kuuweka mji wetu katika hali ya usafi,” alisema Shayo.
Aliongeza kuwa kwa sasa baadhi ya maeneo yameanza kukumbwa na uchafu kutokana na taka kutokusafirishwa kwa wakati, jambo ambalo linaathiri sifa ya Moshi kama mji safi.
“Changamoto kubwa iliyopo ndani ya Manispaa ya Moshi ni kutokuzolewa kwa taka kwa wakati. Taka zinazozalishwa majumbani na viwandani huzolewa, lakini si kwa wakati unaofaa. Nipeni kura niende nikafuatilie hili kwenye halmashauri,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Faraji Swai, alisema ana imani kuwa Shayo ni chaguo sahihi kwa wana-Moshi na ataipeperusha vema bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.
“Nina imani na mgombea wetu. Ni kijana mwenye maono na atawatumikia wananchi kwa bidii kubwa. Tuna uhakika atatuwakilisha vizuri,” alisema Swai.




















