MGOMBEA UDIWANI KATA YA KALOLENI AAHIDI KUIMARISHA MIUNDOMBINU YA BARABARA, ELIMU

KALOLENI – MOSHI.

Mgombea udiwani wa Kata ya Kaloleni kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Nasibu Mariki, amesema iwapo atachaguliwa kushika nafasi hiyo, kipaumbele chake kikuu kitakuwa ni kuimarisha miundombinu ya barabara katika kata hiyo, hasa zile za ndani.

Akizungumza leo septemba 18,2025, kwenye mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni za diwani huyo,  uliofanyika katika viwanja vya Kaloleni Muslim, Mariki alisema kuwa changamoto ya barabara ndicho kilichomsukuma kugombea nafasi hiyo kwa mara nyingine.

"Nawaombeni wananchi wa Kaloleni mniamini na kunichagua, nitahakikisha barabara zote za ndani zinajengwa kwa kiwango cha changarawe ili ziweze kupitika misimu yote ya mwaka,” alisema Mariki.

Mbali na barabara, Mariki alieleza kuwa ana mpango wa kusimamia ujenzi wa ukuta katika shule ya msingi Kaloleni, kukamilisha bwalo la chakula ambalo limebakia kufungwa vioo na kuweka vigae (tiles), pamoja na kukarabati madarasa chakavu kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza ufaulu wa wanafunzi.

Kwa upande wa sekta ya elimu ya sekondari, Mariki alieleza kuwa ataiwasilisha hoja katika Baraza la Madiwani ili shule ya sekondari ya Msasani ijengewe jengo la utawala, kwani kwa sasa shule hiyo inatumia madarasa kama ofisi.

“Tutaiomba serikali kupitia halmashauri ijenge jengo maalum la utawala katika shule ya sekondari Msasani, pia tutahakikisha shule hiyo pamoja na sekondari mpya zinajengewa uzio kwa ajili ya usalama,” alieleza.

Katika sekta ya ulinzi, Mariki alisema atasimamia ukarabati wa kituo cha polisi cha kata hiyo, na kuimarisha kikosi cha Polisi Jamii, ili kuhakikisha usalama kwa wakazi wa Kaloleni unaimarika zaidi.

Akizungumzia kuhusu sekta ya kilimo, mgombea huyo aliahidi kuwa atasimamia upatikanaji wa pembejeo za ruzuku kwa wakulima wa mpunga katika kata hiyo.

Pia, aliahidi kuhakikisha kuwa vikundi halali vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vinanufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa mujibu wa sheria.

"Tutahakikisha fedha hizo za asilimia 10 zinaenda kwa walengwa halali, ili ziweze kuwainua kiuchumi na kuongeza mzunguko wa fedha katika jamii yetu,” alisema Mariki.











Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.