IBRAHIM SHAYO AHAIDI KUFUFUA VIWANDA MOSHI MJINI AKIPEWA RIDHAA

MOSHI-KILIMANJARO.

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kupitia chama cha mapinduzi (CCM), Ibrahim Shayo, amesema kuwa endapo atachaguliwa kuwa mwakilishi wa wananchi bungeni, atahakikisha anapambana kufufua viwanda ambavyo vimesimama kufanya kazi kwa muda mrefu, hususan katika eneo hilo.

Akihutubia septemba 17,2025 kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya NHC, Kata ya Mfumuni, Shayo alisema atashawishi serikali kuwekeza tena katika viwanda vya zamani ili kuleta ajira kwa vijana na kuchochea uchumi wa ndani.

"Tanga wanalima zao la mkonge kwa wingi sana, hapa Moshi tulikuwa na kiwanda cha magunia, lakini sasa kimekufa, mkinipa ridhaa yenu kuwa Mbunge wenu, nitakwenda kupeleka hoja bungeni ili kiwanda hiki kifufuliwe," alisema Shayo.

Aidha, aliongeza kuwa mkoa wa Kilimanjaro, na hasa jamii ya Wachagga, wanasifika kwa matumizi makubwa ya nyama, na hivyo kuna uhitaji mkubwa wa viwanda vya ngozi ili kutumia rasilimali zinazopatikana.

"Wachagga wanasifika kwa kula nyama sana, ng’ombe zinazochinjwa hapa Kilimanjaro ni nyingi, nitapigania kufufuliwa kwa kiwanda cha ngozi ili kuongeza thamani ya mazao ya mifugo na kutoa ajira kwa wananchi wetu," aliongeza.

Shayo alisisitiza kuwa atashirikiana kwa karibu na serikali kuhakikisha viwanda vilivyokufa Moshi vinafufuliwa na kuanza tena uzalishaji, hatua ambayo itasaidia kupunguza tatizo la ajira na kuinua pato la mkoa.



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.