MFUMUNI-KILIMANJARO.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Moshi Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ibrahim Mohamed Shayo, amesema moja ya vipaumbele vyake vikuu endapo atachaguliwa ni kuhakikisha ukuaji wa sekta ya michezo, sanaa na utamaduni unapata msukumo mpya katika Manispaa ya Moshi.
Shayo aliyasema hayo leo Septemba 17, 2025, wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika kata ya Mfumuni, ambao ulienda sambamba na kumnadi mgombea wa nafasi ya udiwani wa kata hiyo Stuart Nathael.
Katika hotuba yake, Shayo alisema sekta ya michezo na sanaa imekuwa ikipuuzwa kwa muda mrefu, licha ya kuwa na nafasi kubwa ya kuwainua vijana kiuchumi na kijamii, na kuleta ajira kwa kupitia vipaji vyao.
"Nikichaguliwa kuwa mbunge wenu, nitashirikiana na wadau wa michezo, sanaa na utamaduni, pamoja na wawekezaji ili kuandaa na kufanikisha mashindano mbalimbali ya michezo kama vile soka, riadha na mpira wa pete, pamoja na shughuli za sanaa na muziki," alisema.
Aliongeza kuwa ni muhimu kuwa na mazingira rafiki ya kukuza vipaji vya vijana kupitia majukwaa ya mashindano na tamasha za kiutamaduni, kwa kuwa Moshi ni mji uliojaa vipaji vya kipekee ambavyo vinahitaji kuibuliwa na kuendelezwa.
"Tutahakikisha tunakuwa na kalenda rasmi ya matukio ya michezo na sanaa kwa mwaka mzima, jambo litakalowapa vijana fursa ya kuonesha vipaji na kujiendeleza," aliongeza Shayo.
Kuhusu masuala ya mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri, Shayo alisema atahakikisha fedha hizo zinatolewa kwa uwazi na kufika kwa walengwa wote, wakiwemo vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
"Mikopo hii si zawadi, ni haki ya kila mwananchi. Nitahakikisha kila mmoja ananufaika na mikopo hii bila ubaguzi, na tunasimamia marejesho yake ili iwe endelevu kwa makundi mengine," alisema.
Shayo alihitimisha kwa kusema kwamba maendeleo ya Moshi hayawezi kufikiwa bila kushirikisha vijana kwa vitendo, hasa kupitia michezo na sanaa, ambayo ndiyo njia kuu ya kuleta mshikamano, ajira, na ustawi wa jamii.










