MOSHI-KILIMANJARO.
Mgombea Udiwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kata ya Mfumuni, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Stuart Nathael, amewaomba wakazi wa kata hiyo kumpigia kura mgombea urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan, katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika Septemba 17, 2025 katika uwanja wa NHC, Kata ya Mfumuni, Nathael alisema serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia imeleta mageuzi makubwa ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo ya elimu, miundombinu na huduma za kijamii.
"Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imeleta mageuzi makubwa siyo tu hapa Kata ya Mfumuni, bali mkoa mzima wa Kilimanjaro na nchi kwa ujumla. Hatuwezi kuacha kumpigia kura kiongozi ambaye ametuletea maendeleo makubwa namna hii," alisema Nathael.
Akiwaomba wananchi wa Mfumuni kumpigia kura kwa muhula mwingine wa miaka mitano, Nathael alitaja miradi kadhaa ya maendeleo iliyotekelezwa kipindi cha uongozi wa Rais Samia, ukiwemo ujenzi wa kumbi tisa za mihadhara katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), pamoja na maktaba ya kisasa yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,000 kwa wakati mmoja.
"Mimi mwenyewe ni miongoni mwa walionufaika kupitia chuo hiki, kwa miaka zaidi ya 40 hatujawahi kuona jengo la ghorofa likijengwa katika kata hii, leo hii, ni historia," aliongeza.
Nathael pia alieleza kuwa ndani ya Manispaa ya Moshi, shule mpya nne za sekondari zimejengwa katika Kata za Bomambuzi, Msranga, Miembeni na Karanga.
Aidha, Shule ya Ufundi Moshi imenufaika kwa kujengewa bweni lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 120 pamoja na vyumba vipya vya madarasa vinane.
Katika Kata ya Rau, serikali imefanikiwa kujenga madarasa mawili mapya, huku akieleza kuwa mradi wa ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi katika Kata ya Mfumuni ambao ulikuwa umekwama, sasa unaendelea baada ya serikali ya CCM kuridhia kutoa zaidi ya Shilingi Bilioni 13 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo.
"Tuna kila sababu ya kumchagua Dk. Samia ili fedha hizi ziletwe na tuweze kukamilisha ujenzi wa stendi yetu, ni lazima tuthamini kazi hii nzuri na kuipigia kura ya ndiyo," alisema.
Nathael alihitimisha kwa kuwasihi wananchi kuhakikisha wanapiga kura tatu kwa mgombea urais, ubunge na udiwani wote kupitia CCM, ili kuendeleza juhudi za maendeleo zilizoanza kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini.













